UN yaripoti kuongezeka vurugu katika jimbo la Upper Nile la Sudan Kusini
Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kwamba timu ya kulinda amani ya umoja huo nchini Sudan Kusini imekuwa ikiripoti kuongezeka vurugu za kijamii pamoja na wizi wa mifugo na uvamizi wa mashamba katika Jimbo la Upper Nile nchini humo.
Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hayo na kuongeza kuwa, matukio hayo ya vurugu katika kaunti za Ulang na Baliet za Jimbo la Upper Nile, kwa mujibu wa serikali za mitaa, yamesababisha vifo vingi na kuwaathiri wanawake na watoto kiasi kwamba yameshapelekea watu wapatao 12,000 kuhama makazi yao.
"Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa na kuongezeka vurugu katika Jimbo la Upper Nile," Dujarric amesema mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa: "Katika kukabiliana na hali hiyo, Timu ya Umoja wa Mataifa Sudan Kusini imetuma vikosi vya kupiga doria huko Baliet wiki hii, ambako maafisa wa kulinda amani walishirikiana na maafisa wa eneo hilo na kutoa msaada wa dharura wa kimatibabu." Itakumbukwa kuwa zaidi ya watu milioni 7.55 nchini Sudan Kusini watakumbwa na utapiamlo wakati wa msimu wa kiangazi utakaoanzia mwezi Aprili na kuendelea hadi Julai mwaka ujao, kipindi ambacho kwa kawaida usambazaji wa chakula unakuwa ni mdogo.
Shirika la Ulinzi wa Usalama wa Chakula (IPC) linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa lilitoa onyo wiki iliyopita likitabiri kwamba njaa itazidi kuwa mbaya katika miezi ijayo Sudan Kusini huku mapigano kati ya makundi hasimu ya kisiasa yakiongezeka na misaada ya kimataifa ikipungua. Tathmini hiyo imekuja huku nchi hiyo ikikaribia kutumbukia upya kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kuzuka mgogoro baina ya Rais Salva Kiir na Makamu wake wa Kwanza, Riek Machar, ambaye hivi sasa anakabiliwa na kesi ya uhaini kama ilivyotangaza serikali ya Salva Kiir.