Mohsein Rezaei: Israel inaharakisha anguko lake kwa kuwauwa makamanda wa Muqawama
-
Mohsen Rezaei
Kamanda Mkuu wa zamani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameonya kuwa mauaji yanayofanywa na utawala wa Israel dhidi ya makamanda wa Muqawama yanaharakisha kuangamia utawala huo.
Mohsen Rezaei ameeleza haya katika shughuli ya mazishi yaliyofanyika leo katika mji wa Kerman kusini mashariki mwa Iran kwa ajili ya kuwaenzi mashahidi wa vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran.
Amesema kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unadhani kuwa unaweza kuendeleza ajenda yake kupitia mauaji lakini ukweli ni kuwa unapiga hatua mbele kuelekea anguko lake kwa kila kamanda mmoja wa Muqawama anayeuawa shahidi.
Mohsein Rezaei ambaye sasa ni mwakilishi wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesisitiza kuwa viongozi wa Muqawama hawakuwa wakiziwakilisha serikali au majimbo. "Makamanda hao walikuwa wawakilishi wa nchi na wananchi waliodhulimiwa", amesema Mohsen Rezaei na kuongeza: Kwa hiyo, kuuliwa kwao shahidi hakuwezi kufumbiwa macho na wananchi.
Kamanda Mkuu wa zamani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameeleza haya baada ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon kuthibitisha kuuawa shahidi kamanda wake wa ngazi yake, Haytham Ali Tabatabai na wanachama wengine wanne wa harakati hiyo katika shambulio la anga la Israel kusini mwa Beirut.
Rezaei amesisitiza kuwa licha ya mashinikizo yasiyokoma ya Israel, Mhimili wa Muqawama nchini Lebanon "hii leo una nguvu zaidi kuliko wakati wa Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah," akimaanisha Katibu Mkuu wa zamani wa Hizbullah, ambaye aliuawa shahidi katika shambulio la Israel dhidi ya mji mkuu wa Lebanon mwaka jana.