Venezuela: Tutatoa jibu kali kwa uvamizi wowote wa Marekani dhidi yetu
-
Venezuela: Tutatoa jibu kali kwa uvamizi wowote wa Marekani dhidi yetu
Waziri wa Ulinzi wa Venezuela amesema kuwa, nchi yake imesimama kidete dhidi ya vitisho vyote vya hivi karibuni vya kijeshi vya Marekani.
Vladimir Padrino Lopez amesisitiza kuwa, hakuna uwepo wa kijeshi wa Marekani au kutumwa kwake kunakoweza kudhoofisha hata chembe moja ya uhuru wa nchi na mamlaka ya kitaifa.
Akizungumza leo, Waziri wa Ulinzi wa Venezuela Vladimir Padrino Lopez ametoa matamshi makali na kuitaja Marekani kuwa "moja ya tawala zenye uharibifu mkubwa zaidi katika historia ya binadamu" . Aidha amesema: "Wanatutishia kwa mabomu, meli za makombora na manowari za nyuklia katika Karibiani, lakini sisi si watumwa wa utawala wowote na tutajibu kwa heshima na ujasiri."
Pia ameshutumu maneva ya kijeshi ya hivi majuzi ya jeshi la majini la Marekani huko Trinidad na Tobago (karibu na pwani ya Venezuela) na kusisitiza kuwa, hakuna mamlaka yoyote ya kigeni inayoweza kunyang'anya uhuru na mamlaka ya kujitawa Venezuela.
Hiivi karibuni Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro alisisitiza kuwa ulimwengu mzima unafahamu kuwa mabepari wanaotawala Marekani wanataka kupora mafuta, gesi na dhahabu ya nchi yake.
Hivi karibuni Marekani ilituma meli ya kivita ya kubeba ndege, USS Gerald R. Ford , ambayo ndiyo kubwa zaidi duniani, pamoja na meli zingine tano za kivita kwenda Amerika ya Kusini, hatua ambayo imekosolewa vikali na Venezuela ikiitaja kuwa ya kichokozi, hatarishi, na kinyume cha sheria za kimataifa.
Tangu Septemba, Washington imeendesha mashambulizi kadhaa dhidi ya meli za kiraia na za uvuvi katika Bahari ya Karibiani, ikidai zinahusiana na biashara ya dawa za kulevya bila kutoa ushahidi wowote.