Israel yatenda jinai nyingine kwa kumuua shahidi kamanda wa Hizbullah
-
Israel yatenda jinai nyingine kwa kumuua shahidi kamanda wa Hizbullah
Utawala vamizi wa Israel umetenda jinai nyingine kwa kumuua shahidi Haitham Ali Tabatabaei kamanda wa ngazi ya juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon.
Hizbullah sambamba na kuthibitisha jinai hiyo imetangaza kuwa, Kamanda Haitham Ali Tabatabaei aliuawa shahidi katika shambulio la utawala wa Israel katika viunga vya kusini mwa Beirut.
Taarifa ya Hizbullah imesema: "Baada ya miaka mingi ya jihadi, uaminifu, na ikhlasi, ameungana na ndugu zake mashahidi na maisha yake yenye baraka ya kujitolea katika njia ya muqawama na kusimama kidete hayakusimama hadi dakika ya mwisho ya uhai wake."
Hizbullah imesisitiza kuwa, Tabatabai alikuwa na nafasi ya kimsingi katika kuimarisha misingi ya muqawama wa Lebanon tokea siku za mwanzo kabisa za kuasisiwa kwake, na kupitia juhudi zake zisizo na kikomo, aliigeuza harakati hiyo kuwa imara na ya ushindi dhidi ya adui.
Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran katika radiamali yake ya kuuawa shahidi Haitham Ali Tabatabaei na utawala wa Kizayuni, aliandika katika mtandao wa kijamii wa "X": Katika usiku wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Bibi Fatima Zahra (as), mmoja wa wapiganaji wa kweli wa njia ya bibi huyo mwema ameuawa shahidi na Wazayuni pamoja na kundi la wanajihadi wenzake.
Wakati huo huo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imelaani shambulizi la anga la utawala wa Israel katika eneo la makazi ya watu katika viunga vya mji wa Beirut na mauaji ya Haitham Ali Tabatabaei, kamanda mwandamizi wa muqawama wa Lebanon na kulitaja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa usitishaji vita na jinai ya kivita na kutaka kufunguliwa mashtaka ya kimataifa wahusika wa jinai hiyo.