UNRWA yatahadharisha kuhusu njaa ya kupanga huko Gaza
-
Kituo cha UNRWA kilichoharibiwa na Israel
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetahadharisha kuhusu hali mbaya ya njaa, kusitishwa huduma muhimu na tishio la maisha ya mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza, likitaja ukosefu mkubwa wa rasilimali za kifedha na vikwazo vikubwa vya utawala wa Israel.
UNRWA imetangaza kuwa sera ya Israel ya njaa ya kimuundo katika Ukanda wa Gaza bado inaendelea na kwamba ukosefu mkubwa wa rasilimali za kifedha umesababisha mgogoro wa binadamu katika eneo hilo kwa kiwango kisicho na kifani.
Adnan Abu Hasna, mshauri wa vyombo vya habari wa UNRWA, amesema kwamba mgogoro wa chakula ni sehemu tu ya matatizo makubwa yaliyopo huko Gaza, akisisitiza kuwa: Mamilioni ya wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi, Syria, Lebanon na Jordan wanasumbuliwa na madhara makubwa katika sekta za elimu, afya na udhamini wa kifedha, sambamba na uhaba wa chakula.
Abu Hasna amesema, mashinikizo na vikwazo vilivyowekwa na utawala wa Israel dhidi ya shughuli za UNRWA vimelifikisha shirika hilo kwenye ukingo wa kuporomoka.
Msemaji wa vyombo vya habari wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa amesema kuwa Israel ndio kikwazo kikuu cha kuingia misaada ya kibinadamu Ukanda wa Gaza, na kuongeza: "UNRWA ina uwezo kamili wa kuwasaidia watu wa Gaza, lakini vikwazo vikali vya serikali ya Tel Aviv haviruhusu uwezo huu kutumika.."
Sambamba na tahadhari hiyo ya Umoja wa Mataifa, utawala wa Kizayuni wa Israel unaendeleza mashambulizi na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, licha ya kutangaza usitishaji wa vita.