Mamluki wa kigeni wana jukumu gani katika kuchochea vita nchini Sudan?
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133562-mamluki_wa_kigeni_wana_jukumu_gani_katika_kuchochea_vita_nchini_sudan
Kamati ya Uchunguzi wa Haki za Binadamu imetangaza kuhusu ushirikiano uliopo kati ya mamluki wa kigeni na Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan RSF katika vita vya ndani nchini humo.
(last modified 2025-11-25T02:39:54+00:00 )
Nov 25, 2025 02:39 UTC
  • Mamluki wa kigeni wana jukumu gani katika kuchochea vita nchini Sudan?

Kamati ya Uchunguzi wa Haki za Binadamu imetangaza kuhusu ushirikiano uliopo kati ya mamluki wa kigeni na Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan RSF katika vita vya ndani nchini humo.

Selma Sassi, Ripota Maalum kuhusu Wakimbizi, Watafuta Hifadhi, Wakimbizi wa Ndani na Wahamiaji Barani Afrika amesema: "Kwa mujibu wa nyaraka zilizokusanywa na Kamati ya Uchunguzi wa Haki za Binadamu, raia wa kigeni wenye silaha wanashirikiana na Vikosi vya Msaada wa Haraka katika vita na jeshi la Sudan." Ameongeza: "Wapiganaji hawa wa kigeni wanazungumza lahaja zisizo za Kisudan na inaaminika waliingia Sudan kutokea nchi jirani, lakini kamati hii hadi sasa haijaweza kuthibitisha uraia wa wapiganaji hao au uhusiano wao na mashirika maalum."

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa awali lilitangaza kuundwa kwa kamati ya kutafuta ukweli kuhusu jinai dhidi ya raia katika mji wa Fasher nchini Sudan.

Hadi sasa, vita vya nchi hiyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 40,000 na kuibua mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani ambapo zaidi ya watu milioni 14 wamekimbia makazi yao. Wakati huo huo, hali ya Fasher ni mbaya na mauaji yanaendelea.

Ingawa habari za kuwepo mamluki wa kigeni katika vita hivyo zilikuwa tayari zimetangazwa katika miezi ya huko nyuma, lakini sasa ripoti za Kamati ya Kutafuta Ukweli Kuhusu Haki za Kibinadamu zimethibitisha rasmi suala hili, na zinaonyesha wazi zaidi kuliko huko nyuma kwamba Sudan imekuwa uwanja wa ushindani na uingiliaji wa wahusika wa kikanda na kimataifa.

Ushahidi uliopatikana kutokana na lahaja za wapiganaji hao zisizo za Sudan unatilia nguvu uwezekano wa kuwepo vikosi vya kigeni kutoka nchi jirani. Suala hili linathibitisha kuwa Sudan haikabiliwi tena na mzozo wa ndani, bali na mtandao wa maslahi ya kigeni na uingiliaji ambao unaweza kufanya mchakato wa vita kuwa mrefu na mgumu zaidi. Ingawa kamati ya kutafuta ukweli bado haijaweza kubainisha utaifa wa watu hao, lakini suala hilo lenyewe linaashiria utata wa vita vya Sudan. Uwepo wa askari wasiojulikana na wasioweza kutambulika hufanya iwe vigumu kuwajibishwa kisheria wahusika na hivyo kuwa sababu ya kuendelea vurugu na ukiukwaji wa haki za binadamu katika pembe tofauti za dunia.

Uharibifu katika mji wa al-Fasher

Uingiliaji wa kigeni nchini Sudan una sababu kadhaa. Kwanza, nafasi ya kijiografia ya Sudan katika Bahari Nyekundu na ukaribu wake na Pembe ya Afrika umeifanya nchi hiyo kuwa nukta ya kimkakati kwa madola ya kikanda na kimataifa. Pili, maliasili ya Sudan. Sudan ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika. Pia, nchi hii ina akiba ya shaba, chokaa, chumvi, jasi na madini mengineyo. Pia, kutokana na kupitia nchini humo Mto Nile, Sudan ina ardhi tajiri yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, ambapo huko nyuma nchi hii ikijulikana kama ghala la chakula la bara la Afrika.

Tatu, machafuko ya kisiasa ya ndani. Kwa miaka mingi, Sudan imekuwa ikikabiliwa na migogoro mikali ya ndani na vita vya wenyewe kwa wenyewe, vikiwemo vita vya muda mrefu huko Darfur na kisha kujitenga kwa Sudan Kusini mwaka 2011. Hali hii imepelekea mataifa mengi ya kigeni kuingia nchini humo kwa visingizio tofauti vikiwemo vya kujaribu kuleta amani, kukomesha ghasia na kuunga mkono michakato ya amani.

Mambo haya sambamba na hasira ya ndani na matatizo ya kiuchumi yameifanya nchi hii kuwa uwanja wa mashindano ya madola ya kikanda kwa ajili ya kuimarisha ushawishi wao barani Afrika, na hasa katika miaka ya hivi karibuni baada ya kuondolewa madarakani Omar al-Bashir. Nchi jirani kama Misri, Ethiopia na nchi za Kiarabu kama vile UAE na Saudi Arabia zina maslahi tofauti nchini Sudan kutokana na ushindani wa kijiografia na kiuchumi. Kwa mfano, Misri ina wasi wasi kuhusu usalama wa rasilimali zake za maji kutokana na Mto Nile, nayo Ethiopia inakabiliwa na changamoto za pamoja nchini Sudan kutokana na mradi wa Bwawa la Ennahda. Nchi za Kiarabu pia zinashiriki katika miradi ya kiuchumi na kisiasa huko Sudan ambapo tunaweza kuashiria uwekezaji mkubwa wa UAE katika migodi ya dhahabu nchini humo, kuwa moja ya miradi hiyo.

Ingawa wengi walikuwa wameonya juu ya uwepo wa vikosi vya kijeshi vya kigeni katika nchi hii tangu mwanzo wa mgogoro na vita, lakini kwa kushadidi vita, sasa uingiliaji wa wazi na wa siri wa nchi nyingine nchini Sudan umekuwa mkubwa zaidi. Kwa hakika, kila moja ya nchi hizi inaunga mkono pande tofauti kati ya vikosi vya RSF na jeshi la Sudan chini ya uongozi wa Abdul Fattah al-Barhan, na hivyo kuzuia mazungumzo ya amani nchini humo. Kwa hakika, tamaa ya nchi za kigeni imefanya kuwa vigumu kutatua mgogoro wa nchi hii, kadiri kwamba wengi wameonya kuhusu uwezekano wa kusambaratika nchi nzima.

Mgogoro wa Sudan umezidi kuwa kitendawili chenye sura nyingi. Ushindani wa ndani, uwepo wa mamluki wa kigeni na uingiliaji wa wachezaji mbalimbali umegeuza mgogoro huu kutoka tatizo la ndani kuwa suala la kimataifa lenye kutia wasiwasi mkubwa. Katika hali hiyo, mustakabali wa Sudan unahitajia zaidi ya suluhisho la haraka la kisiasa, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa kina wa kijamii na kiuchumi, kurejesha imani kati ya wananchi na serikali na kuendelea na juhudi za kuimarisha taasisi za serikali na za kiraia. Kwa njia hii, ikiwa majeshi ya ndani ya Sudan yatafuata njia ya amani na kufahamu vyema maslahi yao ya pamoja, nchi hii inaweza kuondokana na mgogoro huu na kuelekea kwenye mustakabali bora zaidi.