Makubaliano ya dola bilioni 1.4 ya kufufua reli ya TAZARA
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133424-makubaliano_ya_dola_bilioni_1.4_ya_kufufua_reli_ya_tazara
China, Zambia na Tanzania zimesaini makubaliano ya kihistoria ya dola bilioni 1.4 siku ya Alhamisi ya kufufua reli ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
(last modified 2025-11-21T07:57:22+00:00 )
Nov 21, 2025 07:57 UTC
  • Makubaliano ya dola bilioni 1.4 ya kufufua reli ya TAZARA

China, Zambia na Tanzania zimesaini makubaliano ya kihistoria ya dola bilioni 1.4 siku ya Alhamisi ya kufufua reli ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

Reli hiyo ya  kilomita 1,860 kati ya Tanzania na Zambia ilijengwa na China katika miaka ya 1970 ili kurahisisha usafirishaji wa shaba na uagizaji wa mafuta kupitia Tanzania.

Makubaliano hayo yalisainiwa katika mji mkuu wa Zambia, Lusaka, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa China Li Qiang, ambaye pamoja na Rais wa Zambia Hakainde Hichilema na Makamu wa Rais wa Tanzania Emmanuel Nchimbi, walishuhudia sherehe ya uzinduzi wa kufufuliwa kwa TAZARA.

Li alisema TAZARA ni kielelezo cha dhamira ya China ya kukuza uboreshaji wa miundombinu kwa kushirikiana na nchi hizo mbili, na kuongeza kuwa “TAZARA ni mradi wa alama, unaoleta enzi mpya ya maendeleo na ustawi kwa Tanzania, Zambia na China.”

Hichilema alieleza kuwa reli ya TAZARA ni muhimu katika kuibadilisha nchi inayozalisha shaba kwa kiwango cha pili barani Afrika kuwa kitovu cha kikanda cha usafirishaji na vifaa, na kurahisisha ongezeko la biashara, uwekezaji na ajira.

Hichilema alisema: “Tunaona TAZARA si tu kama reli, bali ni njia muhimu ya kiuchumi.”

Nchimbi kwa upande wake alisema: “Mradi huu utaimarisha njia za biashara na kuongeza uagizaji na usafirishaji ili kuunganisha zaidi uchumi wa kikanda.”

Wigo wa kazi za ukarabati unajumuisha marekebisho ya vituo, njia za reli, madaraja na ujenzi wa miundombinu mingine, kwa lengo la kuongeza kiasi cha mizigo kinachosafirishwa kwenye reli hiyo kutoka tani 100,000 hadi tani milioni 2.4 kwa mwaka.

Awali, Hichilema na Li walifanya mazungumzo ya pande mbili kuhusu ushirikiano wa kina wa kimkakati na wa kimaendeleo kati ya nchi hizo mbili, na hatimaye wakasaini makubaliano tisa yanayohusu nyanja mbalimbali.