Araghchi: Iran imejiandaa zaidi kukabiliana na uhasama wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i133432-araghchi_iran_imejiandaa_zaidi_kukabiliana_na_uhasama_wa_israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu sasa imejiandaa kuliko wakati wowote kukabiliana na uhasama wowote kutoka Israel.
(last modified 2025-11-21T08:45:55+00:00 )
Nov 21, 2025 08:01 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi
    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu sasa imejiandaa kuliko wakati wowote kukabiliana na uhasama wowote kutoka Israel.

Katika mahojiano maalumu na gazeti la The Economist tarehe 19 Novemba mjini Tehran, Araghchi amebainisha kuwa uwezo wa makombora ya Iran umeimarika kwa wingi na ubora tangu vita vya siku 12 mezi Juni mwaka huu, na masomo yaliyopatikana yameimarisha ulinzi wa taifa.

Alipoulizwa kuhusu utayari wa Iran iwapo kutatokea mashambulizi mapya ya Israel, Araghchi amejibu kuwa Iran “imejiandaa zaidi kuliko ilivyokuwa katika vita vilivyopita.” Amesisitiza kuwa makombora ya Iran sasa yamepangwa vyema, kwa wingi na kwa ubora. Amesema: “Njia bora ya kuzuia vita ni kuwa tayari kwa vita. Na sisi tuko tayari kikamilifu.”

Kuhusu uhusiano wa Iran na Russia, waziri huyo ameeleza kuwa Moscow ilitoa msaada mkubwa wakati wa vita vya siku 12, hali iliyosababisha kuongezeka kwa ushirikiano baada ya hapo. Aliongeza kuwa Iran inaendeleza zaidi “ushirikiano wa kimkakati” na Russia.

Katika suala la nyuklia, Araghchi amesisitiza kuwa Iran inaunga mkono kufikiwa kwa makubaliano ya nyuklia, lakini lazima yawe “ya haki na yenye uwiano.” Waziri wa Mambo ya Nje aidha amekosoa juhudi za Marekani za kutaka  kulazimisha masharti ya upande mmoja katika mazungumzo. Amesisitiza kuwa urutubishaji wa madini ya urani hauwezi kujadiliwa katika meza ya mazungumzo huku akibaini kuwa Iran iko tayari kuahidi kutotengeneza silaha za nyuklia.

Araghchi amesema: “ Iran haina uzoefu nzuri hata kidogo katika mazungumzo na Marekani.” Hata hivyo, amefafanua kuwa mlango wa mazungumzo bado uko wazi, lakini Iran iko tayari kwa mazungumzo, si kwa masharti ya kulazimishwa.

Zaidi ya miaka kumi iliyopita, Iran na mataifa yenye nguvu duniani walisaini  mkataba wa nyuklia ujulikanao kamaMpango wa Pamoja wa Kina wa Utekelezaji (JCPOA) mnamo Julai 2015 baada ya mazungumzo marefu.

Iran ilikubali kuweka kiwango cha urutubishaji wa uranium kisichozidi asilimia 3.67, kupunguza idadi ya mitambo ya kurutubisha, na kuruhusu ukaguzi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), kwa kubadilishana na kuondolewa kwa vikwazo.

Mnamo Mei 2018, Rais wa Marekani Donald Trump alijiondoa kwenye JCPOA na kurejesha vikwazo, hali iliyosababisha Iran kuzitaka nchi za Ulaya katika mapatano hayo kutekeleza wajibu wao. Hata hivyo, kutokana na mashinikizo ya Marekani, nchi husika za Ulaya hazikutimiza ahadi zao, na Iran ikaanza kupunguza utekelezaji wake taratibu huku ikiongeza urutubishaji wa uranium.

Utawala wa Rais Joe Biden pia ulishindwa kufufua JCPOA, ukiendeleza sera ya vikwazo na kuruhusu makubaliano hayo kudhoofika zaidi.