Makumi wafa maji, 150 watoweka katika ajali ya boti Kongo DR
Makumi ya watu wamethibitishwa kupoteza maisha huku wengine 150 wakitoweka baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Kivu katika mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Duru za habari zinaarifu kuwa, watu 20 wamefariki dunia huku hatima ya wengine 150 ikisalia kitendawili, baada ya boti hiyo kuzama katika Ziwa Kivu usiku wa kuamkia jana Jumanne.
Afisa mmoja wa jimbo la Kivu Kusini amesema, watu zaidi ya 30 wameokolewa, na kwamba sababu ya kuzama kwa boti hiyo bado haijajulikana.
Ajali za boti zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara DRC, na sababu kuu ya ajali hizo ni boti kujaza watu kupita kiasi na ubovu wa boti zenyewe.
Aghalabu ya wananchi wa Kongo DR, nchi yenye misitu mingi inayoyahifadhi makundi ya waasi, hulazimika kutumia usafiri wa boti kwenye maziwa na mito, katika safari za masafa marefu.
Mei mwaka jana, watu 49 walipoteza maisha baada ya boti kuzama mtoni kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.