Mchuano mkali katika uchaguzi mkuu nchini Malawi
Wananchi wa Malawi leo wamejitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu ambapo rais Peter Mutharika anakabiliwa na ushindani mkali.
Mutharika, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2014,amekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa aliyekuwa naibu wake Saulos Chilima na mhubiri wa zamani wa Lazarus Chakwera.
Vituo vya upigaji kura vilifunguliwa mwendo wa saa 12 asubuhi majira ya nchi hiyo, na inatarajiwa kuwa wapiga kura milioni 6.8 waliosajiliwa watashiriki kwenye uchaguzi huo wa rais, wabunge na madiwani katika vituo 5,000 katika nchi hiyo.
Rais Mutharika mwenye umri wa miaka 78 anapongezwa kwa kutekeleza mpango wa ustawi wa a miundombinu na alipunguza viwango vya mfumuko wa bei ya bidhaa nchini humo katika muhula wake wa kwanza madarakani. Lakini wapinzani wake wanamtuhumu kuwa ameshindwa kukabiliana na ufisadi na kwamba anatekeelza sera za upendeleo, madai ambayo Mutharika anakanusha.

Chilima mwenye umri wa miaka 46 na ambaye ni mkuu wa zamani wa kampuni ya mawasiliano, alijiondoa kwenye chama cha Mutharika Democratic Progressive Party mwaka uliopita na akaanzisha chama chake ili kushindana na Mutharika.
Naye Chakwera ambaye ana umri wa miaka 64 alishindwa na Mutharika katika uchaguzi uliopita mwaka 2014 na ili kuimarisha nafasi yake ya ushindi, mara hii amejiunga na rais aliyekuwa mtangulizi wa Mutharika Joyce Banda.
Uchaguzi huu ni wa kwanza tangu kuanzishwa sheria mpya inayohimiza vyama kutangaza mchango mkubwa na kupiga marufuku mazoea ya wagombea wa kutoa fedha kwa raia.