Tume ya uchaguzi Malawi yamtangaza Mutharika mshindi rasmi wa uchaguzi wa urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131214-tume_ya_uchaguzi_malawi_yamtangaza_mutharika_mshindi_rasmi_wa_uchaguzi_wa_urais
Tume ya Uchaguzi ya Malawi imemtangaza aliyekuwa rais wa nchi hiyo Peter Mutharika wa chama cha Democratic Progressive Party (DPP) mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Septemba 16.
(last modified 2025-10-22T06:10:45+00:00 )
Sep 25, 2025 06:41 UTC
  • Tume ya uchaguzi Malawi yamtangaza Mutharika mshindi rasmi wa uchaguzi wa urais

Tume ya Uchaguzi ya Malawi imemtangaza aliyekuwa rais wa nchi hiyo Peter Mutharika wa chama cha Democratic Progressive Party (DPP) mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Septemba 16.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa tume hiyo Annabel Mtalimanja jana Jumatano, Mutharika, ambaye alikuwa rais wa tano wa Malawi kuanzia mwaka 2014 hadi 2020, alishinda kwa kunyakua kura milioni 3 (asilimia 56.8) na kumshinda rais wa sasa Lazarus Chakwera, aliyepata kura milioni 1.77 (asilimia 33).

Kulikuwa na wagombea 17 katika uchaguzi huo wa urais, akiwemo Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Malawi Dalitso Kabambe, aliyeibuka wa tatu kwa kupata kura 211,413 (asilimia 4). Rais wa zamani Joyce Banda yeye alipata kura 86,000 (asilimia 1.6).

Watu wasiopungua milioni 7.2 walikuwa wamesajiliwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Malawi 2025, lakini walioshiriki kwenye uchaguzi ni milioni 5.5 (asilimia 76).

Mutharika, profesa wa sheria mwenye umri wa miaka 85, alimchagua Mwanasheria Mkuu wa zamani na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi, Jane Ansah, 69, kuwa mgombea wake mwenza.

Kufuatia tangazo la Jumatano la Tume ya Uchaguzi, Rais-mteule Mutharika ataapishwa ndani ya siku saba kuanzia Septemba 24, na siyo zaidi ya siku 30 kuanzia tarehe hiyo, wakati matokeo yalipotangazwa rasmi.

Mapema jana hiyohiyo, rais anayeondoka madarakani Chakwera, mwenye umri wa miaka 70, alikiri kushindwa na Mutharika na akasema tayari ameshampongeza rais-mteule.../