Malawi yatangaza mlipuko wa polio baada ya kugundua sampuli za ugonjwa huo
-
Mlipuko wa polio Malawi
Serikali ya Malawi imetangaza kuibuka virusi vya polio aina ya 2 (cVDPV2) kufuatia kugunduliwa kwa sampuli za mazingira.
Dan Namarika Katibu wa Afya na Usafi wa Mazingira katika Wizara ya Afya ya Malawi amesema kuwa virusi vya ugonjwa wa polio vimegunduliwa kupitia ufuatiliaji wa kawaida wa maji taka katika maeneo mawili katika jiji la kibiashara la Blantyre.
Wizara ya Afya ya Malawi imetahadharisha kuwa virusi hivyo husababisha hatari kubwa za kiafya na vinaweza kusababisha ulemavu usioweza kurekebishwa, hasa kwa watoto, sawa na virusi vya polio mwitu.
Namarika ameongeza kuwa: Wizara hiyo inachukua hatua ili kudhibiti mlipuko huo kama walivyofanya mwaka 2022. "Hivyo basi tunawahimiza wananchi kwa ujumla kudumisha tahadhari za usafi wa chakula ili kuzuia kuenea kwa virusi hivyo na kuhakikisha kuwa watoto wamechanjwa kikamilifu,” amesema Namarika Katibu wa Afya na Usafi wa Mazingira katika Wizara ya Afya ya Malawi.
Malawi kwa mara ya mwisho ilikabiliana na ugonjwa wa poliso baada ya kutokea mlipuko wa virusi mwitu vya ugonjwa huo aina ya kwanza mwaka 2022.
Mwezi Februari 2022, baada ya miaka 30 pasina na uwepo wa kesi yoyote ya polio; Malawi ilitangaza mlipuko wa ugonjwa huo baada ya mtoto wa miaka 14 kuripotiwa kuwa na ugonjwa huo.
Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limekuwa likishirikiana na serikali ya malawi katika mapambano dhidi ya polio.
Hii ni katika hali ambayo, mbali na kupata dozi milioni 6.8 za chanjo, UNICEF pia imesaidia kuimarishwa kwa huduma endelevu ya utoaji nchini humo.
Ugonjwa wa polio huathiri mfumo wa neva na sipodhibitiwa unaweza kusababisha ulemavu wa mwili.