Mvua kubwa na radi yaua watu 14 nchini Malawi
Radi imeua watu 14 nchini Malawi katika muda wa wiki mbili zilizopita, huku nyumba 8,000 zikiharibiwa na kubomoka katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Afrika kufuatia kushtadi mvua kubwa nchini humo.
Wilson Molen Kamishna wa Idara ya Kukabiliana na Maafa na Majanga Mbalimbali ya Malawi (DoDMA), ameeleza kuwa vifo na uharibifu huo vimeripotiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Molen amesema idara hiyo ya kukabiliana na maafa inafanya juhudi kubwa kutoa misaada ya kibinadamu kwa wananchi wote waliosalia bila ya makazi kufuatia mvua kubwa zilizoiathiri Malawi.
Aidha amewatola wito wananchi kuendelea kuchukua tahadhari wakati huu ambapo mvua zinaendelea kunyesha ili kuepuka maafa zaidi.
Mwaka jana wakati kama huu, watu wanane waliaga dunia na nyumba elfu kumi zilizoharibiwa kutokana mvua kubwa zilizoathiri Malawi.
Mwaka 2023 pia, kimbunga kwa jina la Freddy kiliua maelfu ya watu kusini mwa Malawi na kupelekea mamilioni ya wengine kukosa makazi. Malawi hadi sasa haijapata nafuu ya kiuchumi kufuatia kimbunga hicho cha Freddy.
Malawi imeathiriwa na uhaba mkubwa wa chakula miaka miwli iliyopita na mwezi jana Rais wa Arthur Peter Mutharika alitangaza hali ya janga la kitaifa katika wilaya zote 26za nchi hiyo na kuomba misaada ya kibinadamu kutoka kwa wafadhili.