WHO kutangaza karibuni kuwa Afrika imetokomeza ugonjwa wa Polio
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53783-who_kutangaza_karibuni_kuwa_afrika_imetokomeza_ugonjwa_wa_polio
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa huenda likatangaza karibuni hivi kuwa bara Afrika halina tena ugonjwa wa kupooza wa Polio.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 29, 2019 03:35 UTC
  • WHO kutangaza karibuni kuwa Afrika imetokomeza ugonjwa wa Polio

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa huenda likatangaza karibuni hivi kuwa bara Afrika halina tena ugonjwa wa kupooza wa Polio.

Mkurugenzi wa WHO barani Afrika, Matshidiso Moeti amesema, "Mambo yakienda yanavyokwenda hivi sasa, kuna uwezekano mkubwa tukatangaza mapema mwakani kuwa bara Afrika limefanikiwa kutomokeza maambukizi ya Polio."

Amesema WHO itatoa tangazo hilo iwapo tu 'mabaki' ya ugonjwa huo ambayo mara ya mwisho yaliripotiwa nchini Nigeria miaka mitatu iliyopita hayataibuka tena.

Kesi ya mwisho ya ugonjwa wa Polio barani Afrika iliripotiwa nchini Nigeria Agosti mwaka 2016. Hata hivyo Aprili mwaka uliofuata wa 2017, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) yalizindua kampeni ya chanjo ya aina yake kuwahi kufanyika katika bara la Afrika dhidi ya Polio, iliyolenga watoto milioni 116 katika nchi 13 za Afrika Magharibi na Kati.

Mtoto wa Kiafrika akipewa chanjo ya Polio

Nchi hizo 13 ni Benin, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Kodivaa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea, Liberia, Mali, Mauritania, Niger, Nigeria na Sierra Leone.

Ugonjwa wa kupooza wa Polio ambao aghalabu huwakumba watoto wenye umri wa miaka mitano hauna tiba, lakini kuna chanjo ya kuuzuia.