WFP: Zimbabwe inakabiliwa na baa kubwa zaidi la njaa
Zimbabwe inakabiliwa na janga baya zaidi la la njaa kuwahi kuikumba nchi hiyo na msaada wa haraka unahitajika ili kunusuru maisha ya mamailioni ya watu.
Hayo yamedokezwa na msemaji wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Herve Verhoosel alipozungumza na waandishi habari mjini Geneva siku ya Jumatano.
Amesema watu milioni 3.6 katika maeneo ya vijijini Zimbabwe hawatokuwa na uhakika wa chakula ifikapo Oktoba mwaka huu na ifikapo Januari mwakani idadi inatarajiwa kuongezeka hadi watu milioni 5.5.
Taarifa zinasema wilaya 60 zinatarajiwa kumaliza akiba yake yote ya mahindi ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu na hii ni sawa na asilimia 60 ya watu wote wa vijijini.
Kwa sasa WFP imesema inatoa msaada wa chakula kwa watu 700,000 mwezi huu wa Agosti na endapo fedha zitaruhusu inatarajia kuongeza idadi ya watu wanaosaidiwa na kufikia milioni mbili mwezi Januari mwakani.
Ili kufanikisha utoaji msaada huo WFP inahitaji dola milioni 173 kutosheleza huduma kwa miezi tisa ijayo. Kwa ujumla jamii ya kimataifa inapaswa kutoa msaada wa dola milioni 331 ili kuisaidia Zimbabwe.
WFP imeomba jumuiya ya kimataifa na wahisani kuchukua hatua haraka ili fedha hizo zipatikane kuweza kunusuru maisha ya mamilioni ya watu na kuepusha janga kubwa.