Ndege ya Tanzania iliyokuwa imezuiwa Afrika Kusini yaruhusiwa kurudi nyumbani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55794-ndege_ya_tanzania_iliyokuwa_imezuiwa_afrika_kusini_yaruhusiwa_kurudi_nyumbani
Ndege ya shirika la ATCL la nchini Tanzania aina ya Airbus A220-300 iliyokuwa imezuiliwa nchini Afrika Kusini, imeruhusiwa kurudi nyumbani na Mahakama Kuu ya Gauteng ya mjini Johannesburg.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 04, 2019 10:12 UTC
  • Ndege ya Tanzania iliyokuwa imezuiwa Afrika Kusini yaruhusiwa kurudi nyumbani

Ndege ya shirika la ATCL la nchini Tanzania aina ya Airbus A220-300 iliyokuwa imezuiliwa nchini Afrika Kusini, imeruhusiwa kurudi nyumbani na Mahakama Kuu ya Gauteng ya mjini Johannesburg.

Mahakama Kuu ya Gauteng, Johannesburg nchini Afrika Kusini imeiruhusu ndege ya Tanzania iliyokuwa imezuiwa katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo nchini humo kuondoka.

Ndege hiyo ilizuiwa katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo Agosti 23, 2019 kwa amri ya mahakama hiyo baada ya mkulima Hermanus Steyn kufungua kesi katika mahakama hiyo akidai fidia ya dola milioni 33.

Kikao cha kusikiliza kesi iliyohusu kuzuiliwa ndege ya AirTanzania nchini Afrika Kusini

Naibu Waziri Mambo ya Nje ya Tanzania, Dk Damas Ndumbaro amesema, Serikali ya Tanzania imeshinda kesi hiyo bila kutoa fedha yoyote ambayo aliyetushitaki alitaka Serikali ya Tanzania tuweke fedha dola milioni 33, kama dhamana.

Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba, “Mahakama Kuu ya Gauteng, Afrika Kusini, leo imetoa hukumu na kuamuru kuwa ndege ya AirTanzania iliyokuwa ikishikiliwa nchini humo iachiwe na mlalamikaji alipe gharama za kesi. Tunawashukuru wote kwa uvumilivu wenu.

Taarifa za awali zinasema kwamba ndege hiyo hivi sasa ipo njiani kurejea Dar es Salaam.