Nov 22, 2019 13:31 UTC
  • WHO: Mapigano yanakwamisha mapambano dhidi ya Ebola Kongo DR

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kuwa, vita na mapigano huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanakwamisha jitihada za kutokomeza ugonjwa hatari wa Ebola ambao umeua maelfu ya watu kufikia sasa.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa na Dakta Mike Ryan, Mkurugenzi wa Kitengo cha Kudhibiti Ebola cha shirika hilo la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, kesi saba tu za ugonjwa wa Ebola ziliripotiwa wiki iliyopita, na kwamba ukosefu wa usalama unayumbisha jitihada za kupambana na virusi hivyo hatarishi.

Amesema raia zaidi ya 40 wameuawa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita katika mashambulizi ya makundi ya waasi mashariki mwa DRC, huku akisisitizia haja ya kuimarishwa usalama katika maeneo hayo ili kupiga jeki jitihada za kuitokomeza kikamilifu Ebola.

Hii ni katika hali ambayo, Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hivi karibuni alisema kuwa, ana matumaini makubwa kwamba maambukizi ya maradhi ya Ebola yatamalizika nchini humo kufikia mwisho wa mwaka huu.

Kliniki ya kutibu Ebola mjini Butembo iliposhambuliwa na waasi

Zaidi ya watu 2,200 wamepoteza maisha huku kesi nyingine zaidi ya elfu moja za Ebola zikithibitishwa kutokana na mlipuko mpya wa ugonjwa huo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ikumbukwe kuwa, mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa hatari wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa bara la Afrika.

Tags