Algeria yataka Syria irejeshwe katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59325-algeria_yataka_syria_irejeshwe_katika_jumuiya_ya_nchi_za_kiarabu
Rais wa Algeria ametoa wito wa kurejeshwa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 23, 2020 01:16 UTC
  • Algeria yataka Syria irejeshwe katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

Rais wa Algeria ametoa wito wa kurejeshwa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria ameyasema hayo katika mahojiano na Kanali ya Televisehni ya Rusiya Al-Yaum ambapo sambamba na kutaka kuondolewa marufuku ya muda ya uwanachama wa Syria katika Jumuia ya Nchi za Kiarabu amesema: "Syria ni moja kati ya nchi ambazo ziliasisi jumuiya hii na Algeria haitaki  kuona taifa au nchi yoyote ya Kiarabu ikipata matatizo."

Naye Sabri Boukadoum, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria siku chache zilizopita alisema kusimamishwa uwanachama wa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ni hasara kubwa kwa jumuiya hiyo na nchi za Kiarabu kwa ujumla. Aliongeza kuwa: "Nchi za Kiarabu zinapaswa kuchukua hatua za kivitendo za kuhakikisha Syria inarejea katika Jumui ya Nchi za Kiarabu."

Algeria inatazamiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 32 wa Kiduru wa Kawaida wa Viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ambao umepangwa kufanyika mwishoni mwa Mwezi Machi.

Kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilisamamisha kwa muda uwanachama wa Syria mwaka 2011 baada ya kuanza mgogoro katika nchi hiyo. Hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia mashinikizo ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo nchi kadhaa za Kiarabu pia zilitangaza kukata uhusiano wa kidiplomasia na Syria.

Baada ya Rais Bashar al-Assad wa Syria kufanikiwa kusambaratisha magaidi na njama ya Kiarabu-Kimagharibi, hivi sasa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na nchi nyingine za Kiarabu za eneo zinajaribu kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia na Damascus.