Askari polisi na magaidi 7 wauawa kwenye makabiliano Misri
(last modified Wed, 15 Apr 2020 08:06:52 GMT )
Apr 15, 2020 08:06 UTC
  • Askari polisi na magaidi 7 wauawa kwenye makabiliano Misri

Afisa wa polisi wa Misri na washukiwa saba wa genge la kigaidi wameuawa katika makabiliano ya risasi baina ya pande mbili hizo jijini Cairo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imesema, makabiliano hayo yalitokea jana Jumanne katika wilaya ya al-Amiyira, viungani mwa mji mkuu Cairo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, askari polisi wengine watatu wamejeruhiwa katika mapambano hayo ya risasi, lakini maafisa usalama wamefanikiwa kuwaangamiza magaidi saba, mbali na kutwaa silaha zilizokuwa zinatumiwa nao.

Wiki iliyopita pia, jeshi la Misri lilizishambulia ngome za magaidi katika eneo la Sinai kaskazini mwa nchi hiyo kufuatia kuongezeka mashambulizi ya magaidi. Operesheni hiyo ya maafisa usalama ilijiri siku chache baada ya magaidi kufanya mashambulizi pambizoni mwa eneo la Rafah na kumuua mwanajeshi mmoja wa Misri na kuwajeruhi wawili. 

Kituo cha upekuzi kaskazini mwa Cairo

Makundi ya kigaidi huko Misri yameshadidisha hujuma na mashambulizi yake katika mkoa wa Sinai ya Kaskazini na wakati huo huo pia yanafanya hujuma katika maeneo ya katikati na kusini mwa Sinai na vile vile katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Kundi liitwalo Ansarul Baitul Maqdis ambalo limebadili jina lake na kuwa kundi la Mamlaka ya Sinai baada ya kuungana na kundi la kigaidi la Daesh, ndilo linalotekeleza mashambulizi mengi dhidi ya askari wa Misri. 

Tags