Jun 15, 2020 15:42 UTC
  • Mlipuko mpya wa Ebola waua watu 11 Kongo DR

Huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikiendelea kukabiliana na janga la sasa la virusi vya corona, mlipuko mpya wa virusi vya Ebola umeripotiwa katika mkoa wa magharibi mwa nchi wa Equateur.

Taasisi za afya nchini humo zimetangaza leo Jumatatu kuwa, watu 17 wameambukizwa virusi vya Ebola katika mlipuko huo mpya, ambapo 11 miongoni mwao wameaga dunia.

Mamlaka husika nchini DRC zimesema kuwa, kesi 12 mpya za Ebola ziliripotiwa wiki iliyopita, katika hali ambayo nchi hiyo ya katikati mwa Afrika yenye mfumo dhaifu wa afya inakabiliana na mlipuko wa surua ambao umeshaua watu zaidi ya elfu sita, mbali na janga la corona ambalo limeua watu 112 katika kesi 4,800 za virusi hivyo zilizoripotiwa hadi sasa.

Mapema mwezi huu wa Juni, Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitangaza kuwa, homa ya Ebola imeripotiwa tena katika maeneo ya kaskazini  magharibi mwa nchi, na kwamba tayari watu wanne wameaga dunia katika maeneo hayo kutokana na homa ya virusi hivyo.

Miezi miwili iliyopita Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) alitahadharisha kuhusu uwezekano wa kuibuka mlipuko mpya wa virusi vya homa ya Ebola huko Congo DR. 

Image Caption

 Virusi vya Ebola vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 2,200 nchini DRC tokea mwaka 2018.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikuwa inajiandaa kutangaza kumalizika kabisa ugonjwa huo mwezi Aprili mwaka huu, lakini siku chache kabla ya tangazo hilo WHO ilitangaza habari ya kuthibitishwa kesi nyingine mpya ya ugonjwa huo.

Tags