Waziri Mkuu wa Ethiopia atembelea Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i65096-waziri_mkuu_wa_ethiopia_atembelea_kenya
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed leo ametembelea Kenya na kujiunga na Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo katika ufunguzi wa kituo kipya cha mpakani cha Moyale katika Kaunti ya Marsabit.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 09, 2020 08:42 UTC
  • Waziri Mkuu wa Ethiopia atembelea Kenya

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed leo ametembelea Kenya na kujiunga na Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo katika ufunguzi wa kituo kipya cha mpakani cha Moyale katika Kaunti ya Marsabit.

Punde baada ya Bw. Ahmmed kuwasili, Moyale, alikagua gwaride la heshima la Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) na baada ya hapo akatemebelea kituo hicho cha mpakani akiwa na mwenyeji wake, Rais Kenyatta.

Kituo hicho cha huduma za mpakani, ambacho kinajengwa katika mpaka wa Ethiopia na Kenya katika eneo la Moyale, ni sehemu ya mradi wa barabra ya kilomita 502 ya Howassa-Moyale, ambayo nayo ni sehemu ya mradi mkubwa wa korido ya usafiri ya Mombasa-Nairobi-Addis Ababa.

Gwaride la heshima la Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kwa ajili ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed katika kituo cha mpakani cha Moyale, Kenya

Waziri Mkuu Abiy Ahmed amesema kuzinduliwa kituo hicho ni dhihirisho la wazi la azma ya nchi mbili kuimarisha biashara. Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, wale wanaotaka kuvuka mpaka kutoka nchi mbili sasa watahudumiwa haraka bila kupoteza wakati na hivyo kurahisiha biashara. Inatarajiwa kuwa baada ya uzinduzi wa kituo hicho cha mapakani Rais Kenyatta na Waziri Mkuu Ahmed wataelekea katika Kaunti ya Lamu eneo la pwani kukagua ujenzi wa bandari mpya ya Lamu ambayo ni sehemu ya mradi wa kimataifa wa Bandari ya Lamu-Sudan Kusini- Ethiopia maarufu kama LAPSSET.

Mradi huo uliozinduliwa mwaka 2012 unajumuisha bomba la mafuta kutoka bandari ya Lamu hadi Addis Ababa, reli, barabara, viwanja vya ndege na maeneo ya kitalii. Mradi wa LAPSSET unatazamiwa kuimarisha biashara na mawasiliano baina ya nchi za eneo hilo.