Dec 14, 2020 12:22 UTC
  • UN yatiwa wasiwasi na mapigano Msumbiji; laki 4 wahama makazi yao

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, mgogoro mkubwa wa kibinadamu unanukia kaskazini mwa Msumbiji, ambapo watu zaidi ya laki nne wamelazimika kuyahama makazi yao wakihofia usalama wao.

Shirika la habari la Reuters leo Jumatatu limemnukuu Valentin Tapsoba, Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR kanda ya kusini mwa Afrika akisema kuwa, mgogoro wa wakimbizi kaskazini mwa mkoa wa Cabo Delgado unatazamiwa kuziathiri nchi jirani za Kiafrika.

Mapigano kati ya wanamgambo wenye silaha na wenye misimamo ya kuchupa mipaka na vikosi vya serikali ya Msumbiji yamezusha hofu miongoni mwa raia na kuwafanya wakimbie makazi yao.

Ingawaje serikali ya Msumbiji inakadiria kuwa watu zaidi ya laki tano na 70 elfu wamelazimika kuwa wakimbizi katika mkoa huo unaoshuhudia mapigano ya mara kwa mara, lakini afisa huyo wa UNHCR amesema takwimu zao zinaonyesha kuwa, raia wa Msumbiji waliolaziika kuyahama makazi yao kufikia sasa ni laki nne na 24 elfu.

Ramani inayoonyesha mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado

Katika hatua nyingine, viongozi wa Msumbiji, Tanzania, Afrika Kusini, Zimbabwe na Bostwana wanatazamiwa kukutana kuanzia leo Jumatatu kujadili hali ya usalama na kushadidi vitendo vya kikatili vinavyofanywa na wanamgambo hao kama mauaji, kukata watu vichwa, kuteka nyara na hata kuchoma moto nyumba zilizoko katika mkoa huo wa kaskazini mwa nchi.

Watu zaidi ya elfu mbili wameuliwa katika vijiji vya mkoa huo wa Cabo Delgado ulioko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Oktoba mwaka 2017, kutokana na mashambulizi ya umwagaji damu ya wanachama wa kundi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, ambao wakazi wa maeneo hayo wanawatambua kwa jina la al-Shabaab.

Tags