Mmishonari wa Marekani afungwa miaka 15 kwa kunajisi mayatima Kenya
Raia wa Marekani ambaye alikuwa anafanya kazi kama mmishonari nchini Kenya amehukumiwa kifungo cha zaidi ya miaka 15 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kuwanajisi mabinti mayatima.
Mmishonari huyo wa Kikristo, Gregory Dow ambaye alifungua kituo cha kuhifadhi mayatima nchini Kenya mwaka 2008 pamoja na mkewe, aliikimbia nchi hiyo ya Afrika Mashariki mwaka 2017 baada ya kashfa ya ufuska wake kufichuka.
Mwaka uliopita, Dow alikiri mashitaka manne yaliyokuwa yakimkabili ya kunajisi watoto wadogo katika nchi ya kigeni. Mmishonari huyo anadaiwa kuwabaka mabinti wa hadi miaka 12 katika kipindi cha karibu muongo mmoja cha kuendesha na kusimamia kituo hicho.
Michael Driscoll, afisa wa Polisi ya Federali ya Marekani (FBI) amesema Mmishonari huyo ni mfano hai wa methali ya 'mbwa mwitu aliyevalia ngozi ya kondoo."
Mamishonari wa Marekani wamekuwa wakijihusisha na ufuska wa aina hiyo katika kona mbalimbali za dunia. Mwaka 2018, mmishonari mwingine wa Marekani kutoka jimbo la Arkansas alihukumiwa kifungo cha miaka 40 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kuwanajisi mabinti wakiwemo wa umri wa miaka sita katika kituo cha mayatima nchini Haiti.
Kwa mujibu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Marekani, takriban makasisi 6,900 wa Kanisa la Katoliki la Roma wanadaiwa kuwalawiti watoto wadogo 16,900 kati ya mwaka 1950 na 2011.