"Unga mkono serikali au jiuzulu", Uhuru amwambia Naibu Rais William Ruto
-
Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya leo Ijumaa amemtaka Naibu Rais William Ruto ajiuzulu, akisema mtu hawezi "kutukana watu" wakati pia anajivunia mafanikio ya serikali.
Rais Kenyatta amemkosoa Naibu wake katika hotuba yake kwenye mkutano wa wafanyabiashara nje ya hospitali mpya ya Uthiru katika Kaunti ya Kiambu. Vilevile amelaani "siasa za mgawanyiko na mtawanyiko" na kusisitiza haja ya kuwaunganisha watu, sio kuwachochea wao kwa wao.
"Tunahitaji kupunguza umaskini. Kwa upande mmoja unasema serikali ni mbaya (unaikosoa serikali kuwa mbaya) na kwa upande mwingine, unajisifu kwa mafanikio yake", amesema Rais Kenyatta akimkosoa Naibu wake William Ruto na kumwambia: "Ikiwa unataka mazuri au mafanikio ya serikali hii, kaa nayo la sivyo, ondoka zako".
Ameongeza kuwa, serikali yake haihitaji maneno matupu na kwamba inataka kuona maendeleo, barabara, kilimo na maendeleo mengine ya ustawi. "Tumeazimia kutayarisha ajira na kuijenga Kenya", amesisitiza Uhuru Kenyatta.
Kabla ya kuelekea Dagoretti, Rais Uhuru Kenyatta alihutubia umati katika mji wa Kikuyu, ambapo pia aliwaomba wananchi kunga mkono mpango maridhiano ya kitaifa wa BBI uliofikiwa baada ya handshake (kupeana mkono) na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM), Raila Odinga.
Amesema: "Msisikilize wapinzani wa BBI, ambao hata hawana suluhisho mbadala."