Wanachuo wa Mauritania wapinga upenyaji wa Wazayuni katika nchi yao
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia nchini Mauritania wametangaza himaya na uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina na kupinga vikali upenyaji na ushawishi wa Wazayuni katika nchi hiyo.
Katika kongamano lao waliloandaa na kulipa jina la"Quds ni amani, na kuanzisha uhusiano na Israel ni usaliti" wanachuo hao wameanzisha kampeni maalum ya "mapambano dhidi ya upenyaji wa Wazayuni na kutetea uadilifu".
Aidha wamesisitiza katika nara zao kuwa, wanafungamana kikamilifu na malengo matukufu ya wananchi wa Palestina na kwamba, muqawama na mapambano ndio njia pekee ya kupata ushindi.
Wanachuo hao wa Mauritania wamesisitiza pia kuwa, wanapinga harakati za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel unaotenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Mwanzoni mwa mwezi huu pia, Maulamaa na Maimamu wa Swala za Jamaa wasiopungua 200 nchini Mauritania walitoa Fatuwa inayorahamisha kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel.
Aidha Harakati za vyama mbalimbali vya kisiasa katika Bunge la Mauritania zenye lengo la kupasishwa sheria itakayopiga marufuku na kutambua kuwa ni uhalifu suala la kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel zinaendelea kushika kasi katika Bunge la nchi hiyo.
Katika miezi mitatu ya mwisho wa mwaka uliomalizika wa 2020, nchi nne za Kiarabu za Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco zilianzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Kizayuni na Israel, hatua ambayo imeendelea kulaaniwa na kukosolewa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.