Mar 07, 2021 07:35 UTC
  • Afrika CDC: Ebola imeua watu 13 Kongo DR na Guinea

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika CDC kimesema idadi ya watu walioaga dunia kutokana na mripuko mpya wa ugonjwa wa Ebola katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Guinea imeongezeka na kufikia watu 13.

Kituo hicho cha Umoja wa Afrika chenye nchi wanachama 55 kilisema hayo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, mbali na vifo, idadi ya watu walioambukizwa maradhi hayo katika nchi mbili hizo za Afrika imeongezeka hadi watu 29.

Taarifa ya Afrika CDC imebainisha kuwa, hadi kufikia sasa, kiwango cha vifo mkabala wa maambukizi DRC na Guinea ni asilimia 45  huku ikitoa mwito kwa wananchi wa nchi mbili hizo  kukumbatia chanjo ya kukabili maandamano hayo.

Kituo hicho kimesema Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufikia sasa imeripoti kesi 11 na vifo vinne.

 

Wananchi wakichanjwa katika mji wa Butembo DRC

Wakati huo huo, idadi ya waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Ebola nchini Guinea sasa imeongezeka na kufikia watu tisa huku waliothibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo hatari wakiwa ni 18.

Haya yanajiri huku nchi mbili hizo zikiendelea na kampeni ya utoaji wa chanjo ya kukabiliana na maradhi hayo hatarishi.

Tags