Rais mpya wa Niger aapishwa baada ya jaribio la mapinduzi
Mohamed Bazoum ameapishwa kuwa Rais mpya wa Niger, siku chache baada ya kujiri jaribio la mapinduzi lililofeli nchini humo.
Kiapo hicho cha jana Ijumaa kinaashiria kufunguliwa ukurasa mpya wa historia, kwani hii ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika kushuhudia makabidhiano ya uongozi kwa njia ya demokrasia, tokea ipate uhuru mwaka 1960.
Usalama uliimarishwa katika mji mkuu Niamey wakati wa hafla hiyo, kwani imekuja siku mbili baada ya vyombo vya usalama nchini humo kuzima jaribio la mapinduzi.
Usiku wa kuamkia Alkhamisi hii, milio mikubwa ya risasi ilisikika karibu na ofisi ya rais wa Niger katika mji mkuu wa nchi hiyo Niamey, lakini masaa kadhaa baadaye maafisa usalama walitangaza kuwa wamezima jaribio la mapinduzi. Serikali ya Niamey imesema watu kadhaa wametiwa mbaroni wakihusishwa na jaribio hilo la mapinduzi.
Nchi hiyo ambayo inahesabiwa kuwa maskini zaidi kwa mujibu wa viwango vya maendeleo vya Umoja wa Mataifa, imeshuhudia mapinduzi manne ya kijeshi, la mwisho likishuhudiwa mwaka 2010.
Bazoum mwenye umri wa miaka 61 na ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani alipata asilimia 55.66 ya kura zilizopigwa katika duru ya pili ya uchaguzi iliyofanyika Februari 21 mwaka huu.
Anaingia madarakani kurithi mikoba ya Mahamadou Issoufou ambaye amemaliza muda wake wa kuongoza, huku kibarua cha kwanza kinachomsubiri kikiwa ni kuimarisha usalama, sambamba na kufufua uchumi wa nchi uliozorota.