"Kuuawa viongozi wa Muqawama hakutadhoofisha mapambano dhidi ya Wazayuni"
(last modified 2024-10-19T07:20:50+00:00 )
Oct 19, 2024 07:20 UTC

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema mauaji ya kigaidi ya viongozi na makamanda wa kambi ya Muqawama hayatadhoofisha mapambano ya taifa hili la Kiislamu dhidi ya dhulma na uvamizi.

Pezeshkian alisema hayo katika ujumbe wake wa jana ya Ijumaa, baada ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS kuthibitisha rasmi kwamba kiongozi wake, Yahya Sinwar ameuawa shahidi wakati wa makabiliano ya moja kwa moja kwenye uwanja wa vita na wanajeshi wa Israel kusini mwa Gaza.

Dakta Pezeshkian amesema, "Adui anapaswa kujua kwamba kuuawa shahidi kwa makamanda, wanamamuqawama na viongozi wao hakutadhoofisha Muqawaa wa taifa la Kiislamu dhidi ya uonevu na uvamizi." 

Ameeleza bayana kuwa, "Kiongozi mmoja anapoanguka (anapouawa), mwingine huinuka." Rais wa Iran amesema hayo akinukuu kauli ya Ismail Haniyeh, kiongozi mwingine wa HAMAS aliyeuawa shahidi na utawala katili wa Israel.

Shahidi Yahya Sinwar

"Shahidi Sinwar (alipambana) kishujaa hadi pumzi yake ya mwisho, na wala hakukata tamaa," ameeleza Rais Pezeshkian huku akirejelea video inazomuonyesha kiongozi huyo wa Muqawama akikabiliana na vikosi vya utawala vamizi wa Israel licha ya kujeruhiwa.

Dakta Pezeshkian ameongeza kuwa, "Kupigana dhidi ya uchokozi na kutoa zawadi ya uhuru na ukombozi kwa wamiliki halali wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni harakati kubwa yenye lengo adhimu ambalo halitasitishwa na mauaji ya mashujaa wake." 

Tags