May 04, 2021 01:33 UTC
  • DRC yadhibiti mripuko wa 12 wa ugonjwa wa Ebola

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza habari ya kudhibitiwa mripuko wa 12 wa ugonjwa wa Ebola nchini humo, miezi mitatu baada ya kesi ya kwanza kuripotiwa katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Hayo yalitangazwa jana Jumatatu na Jean-Jacques Mbungani, Waziri mpya wa Afya wa DRC ambaye alibainisha kuwa, watu sita wameaga dunia kwa maradhi ya Ebola katika mripuko huo wa 12.

Amesema Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kama nchi nyingine duniani hivi sasa inapambana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, na kwamba janga la Corona limekuwa na taathira hasi kwa jitihada za kukabiliana na Ebola nchini humo. 

Katika taarifa ya jana Jumatatu pia, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema, "hii leo (jana Jumatatu) ni mwisho wa mripuko wa 12 wa Ebola nchini DRC. Mripuko huo wa Ebola ambao uliripotiwa mwezi Februari, ulikuja miezi tisa baada ya mripuko mwingine kutangazwa kuwa umemalizika katika mkoa huo huo."

Dakta Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO katika kanda ya Afrika amewashukuru na kuwapongeza wahudumu wa afya katika mkoa huo, kwa jitihada zao za kuudhibiti ugonjwa huo hatari, wakishirikiana na maafisa wa serikali za mitaa.

DRC imekuwa ikikabiliwa na majanga mawili kwa wakati mmoja

Huu ulikuwa mripuko wa nne kuripotiwa katika kapindi cha chini ya miaka mitatu; huku miji ya mkoa wa Kivu Kaskazini iliyoathiriwa zaidi na mripuko huo ikiwa ni Butembo, Byena, Katwa na Musienene.

Dakta Moeti anasisitiza kuwa, ingawaje mripuko huu wa 12 umeweza kudhibitiwa, lakini kuna haja kuendelea kuwa macho na kuchukua hatua za tahadhari. Katika mripuko wa 11, watu 128 walibainika kupatwa na maradhi ya Ebola na wengine 53 waliaga dunia kwa ugonjwa huo katika mkoa huo wa Kivu Kaskazini nchini Kongo DR. 

Tags