Kenya na Burundi zakubaliana kuimarisha uhusiano wa pande mbili
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mwenzake wa Burundi, Evariste Ndayishimiye wamesaini mapatano ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa Nairobi na Bujumbura katika nyuga mbalimbali.
Mapatano hayo yalisainiwa jana mjini Kisumu, magharibi mwa Kenya, ambapo mataifa hayo mawili wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yamekubaliana kuboresha mahusiano yao katika nyuga za kilimo, michezo, utamaduni, biashara na mambo ya nje.
Kadhalika pande mbili hizo zimesisitizia azma yao ya kuiendelea na kuistawisha jumuiya ya EAC.
Marais wa Kenya na Burundi wameafikiana juu ya kuangalia upya makubaliano ya Kamisheni ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano ya mwaka 2018, kwa lengo la kuimarisha zaidi uhusiano wa nchi mbili hizo.
Aidha Kenya na Burundi zimekubaliana kulipa kipaumbele suala la elimu katika mipango yao ya baada ya janga la Corona ambalo linaendelea kuitikisa dunia.
Kenya na Burundi ni nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo mwaka 2010, ilizindua soko la pamoja.