Ayman Nour: Kunyongwa viongozi wa Ikhwani kutazusha machafuko nchini Misri
(last modified Sun, 27 Jun 2021 02:27:51 GMT )
Jun 27, 2021 02:27 UTC
  • Ayman Nour: Kunyongwa viongozi wa Ikhwani kutazusha machafuko nchini Misri

Kiongozi wa chama cha El Ghad nchini Misri ameitaka Kamati ya Kimataifa ya Kuzuia Adhabu ya Kifo katika nchi za Kiarabu kuwasiliana na jumuiya za kimataifa kwa ajili ya kusitisha utekelezaji wa hukumu ya kifo iliyotolewa dhidi ya viongozi kadhaa wa chama cha Ikhwanul Muslimin.

Ayman Nour amesema kamati hiyo imeanza mazungumzo ya mabunge na taasisi za kimataifa ili kuhakikisha serikali ya Misri inasitisha hukumu ya kifo iliyotolewa na mahakama za Misri dhidi ya wapinzani wa serikali.

Kiongozi wa chama cha Ghad amesema anatarajia kwamba harakati hizo ziitazaa matunda.

Siku kadhaa zilizopita Mahakama ya Rufaa ya Misri ambayo uamuzi wake huwa wa mwisho, ilipasisha hukumu ya kunyongwa viongozi 12 wa harakati ya upinzani ya Ikhwanul Muslimin eti kwa kupatikana na hatia ya kuhusika na matukio ya Medani ya Rabia mashariki mwa jiji la Cairo hapo mwaka 2013.

Tarehe 28 Juni mwaka 2013 mamilioni ya Wamisri walikusanyika na kufanya mgomo katika medani hiyo wakipinga hatua ya jeshi la nchi hilo lililokuwa likiongozwa na rais wa sasa wa nchi hiyo jenerali Abddel Fattah al Sisi ya kuipindua serikali ya kwanza kuchaguliwa kwa njia za kidemokrasia ya Misri na kumuondoa madarakani Muhammad Morsi.

Makabiliano baina ya jeshi la Misri na waandamanaji hao yalipelekea kuuawa watu wasiopungua 632. Raia wengine zaidi ya elfu nne walijeruhiwa. 

Tags