Iran na Misri zajadili masuala ya kikanda na kimataifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sisi; ambapo wamejadili masuala muhimu ya kikanda na uhusiano wa pande mbili.
Araghchi alikutana na Rais El-Sisi jana Alhamisi mjini Cairo, Misri ambapo katika mazungumzo hayo, wamejadili kuhusu maendeleo ya kieneo na kusisitiza umuhimu wa kuongezwa juhudi za kukomesha jinai za Wazayuni huko Gaza, kuzuia uvamizi dhidi ya Lebanon, kuwasaidia wakimbizi na kudhibiti uchochezi wa utawala wa Kizayuni. Pia wamekaribisha juhudi za kidiplomasia za Iran.
Araghchi amesema, Iran na Misri zina historia ndefu ya uhusiano wa pamoja wa kiitikadi na kihistoria na hiyo ni fursa nzuri ya kuimarishwa uhusiano wa nchi hizi mbili katika nyuga zote.
Ameeleza bayana kuwa, Iran iko tayari kutumia uwezo wake wote kukomesha mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Palestina hasa Gaza na pia Lebanon.
Kwa upande wake, Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri amepongeza siasa za Jamhuri ya Kiislamu za kuhakikisha inakuwa na uhusiano mzuri na nchi zake jirani na za ukanda huu mzima na kusema kuwa, kuna wajibu wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kuondoa vizuizi vyote vilivyopo ili kufufua uhusiano wa Misri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mapema jana, Araghchi alikutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Misri, ambapo walibadilishana mawazo kuhusu maendeleo ya kikanda, hasa vita vya Gaza na Lebanon. Cairo ni kituo cha nane cha ziara ya kikanda ya Araghchi, ambayo tayari imempeleka Lebanon, Syria, Saudi Arabia, Qatar, Iraq na Oman katika kipindi cha wiki moja iliyopita.