Marekani kuiuzia Misri makombora ya dola milioni 740
Serikali ya Marekani imeidhinisha mauzo ya makombora yenye thamani ya mamilioni ya dola kwa Misri licha ya serikali ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kuendelea kuandamwa na shutuma za ukiukaji wa haki za binadamu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeidhinisha mpango wa kuiuzia Misri makombora ya Stinger kwa gharama inayokadiriwa kuwa ya dola milioni 740.
Aidha Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imetangaza kwamba, tayari imekwishawasilisha nyaraka zinazohitajika kuliarifu Bunge la Congress kuhusu mpango huo.
Kwa mujibu na Wakala wa Ushirikiano wa Usalama wa Ulinzi wa Pentagon (DSCA), Cairo imetuma maombi ya ununuzi wa makombora 720, ikijumuisha zana 20 za PVFT, kwa matumizi ya gari kwenye mifumo iliyopo ya Avenger.
Nchi hiyo ya Kiarabu imesalia kuwa mshirika wa kikanda wa Washington licha ya kukumbwa na madai mengi ya unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na ukandamizaji wa kisiasa chini ya serikali ya Rais Abdel Fattah al-Sisi. Misri inapokea zaidi ya dola bilioni moja za msaada wa kijeshi kutoka kwa Marekani kila mwaka.
Ikumbukwe kuwa, huko nyuma, Marekani ilitishia kuiwekea vikwazo Misri iwapo ingenunua ndege za kivita za Sukhoi-35 kutoka Russia. Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, Marekani ambayo inadhibiti soko la mauzo ya silaha duniani, inawazuia washirika na waitifaki wake kununua silaha za Russia ili ipate fursa ya kuendelea kuhodhi soko hilo.