Wananchi wa Argentina waandamana kuliunga mkono taifa la Palestina
Maandamano makubwa yamefanyika katika mji mkuu wa Argentina, Buenos Aires, huku maelfu ya wananchi wakikusanyika katika baadhi ya barabara kuu na nembo na vituo muhimu vya jiji hilo, kutangaza himaya na uungaji mkono wao kwa taifa madhulumu la Palestina.
Maandamano hayo yaliandaliwa na Kamati ya Mshikamano na Watu wa Palestina ya Argentina, kama sehemu ya kampeni ya kitaifa iliyojumuisha majimbo na miji kadhaa ya Argentina, chini ya kaulimbiu, "Argentina Yapinga Mauaji ya Kimbari huko Gaza."
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba bendera za Palestina pamoja na mabango na maberamu yaliyoandikwa jumbe mbalimbali za kuwaunga mkono Wapalestina, walikusanyika katika maeneo tofauti mjini Buenos Aires na kupiga nara za kulaani jinai za utawala ghasibu wa Israel.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, waandamanaji hao walisikika wakipiga nara za kutangaza kuwa pamoja na taifa la Palestina na wakati huo huo kulaani siasa za kivamizi za utawala dhalimu wa Israel.
Aghalabu wa waandamanaji hao walikuwa wamevalia mavazi mekundu, kuashiria umwagaji damu wa watu wa Palestina na kupinga vitendo vya mauaji ya halaiki vinavyotekelezwa dhidi ya raia wa Gaza.
Maandamano ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kulaani siasa za kibaguzi za utawala wa Kizayuni wa Israel yameendelea kushuhudiwa kila pembe ya dunia na kuzidi kuonyesha kufeli sera za kibaguzi za Israel na waungaji mkono wake.