CDC: Afrika inakabiliwa na mlipuko mbaya zaidi wa kipindupindu katika miaka 25
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133164-cdc_afrika_inakabiliwa_na_mlipuko_mbaya_zaidi_wa_kipindupindu_katika_miaka_25
Shirika la Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (CDC) limetahadharisha kuwa bara la Afrika linakabiliwa na mlipuko mbaya zaidi wa kipindupindu katika kipindi cha robo karne, likifungamanisha ongezeko hilo na miundombinu dhaifu ya maji na migogoro inayoendelea katika sehemu mbalimbali za bara hilo.
(last modified 2025-11-14T06:09:15+00:00 )
Nov 14, 2025 06:09 UTC
  • Africa CDC: Kipindupindu kinaenea kwa kasi Afrika
    Africa CDC: Kipindupindu kinaenea kwa kasi Afrika

Shirika la Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (CDC) limetahadharisha kuwa bara la Afrika linakabiliwa na mlipuko mbaya zaidi wa kipindupindu katika kipindi cha robo karne, likifungamanisha ongezeko hilo na miundombinu dhaifu ya maji na migogoro inayoendelea katika sehemu mbalimbali za bara hilo.

Kwa mujibu wa shirika hilo, zaidi ya visa 300,000 vya kipindupindu na vinavyoshukiwa kuwa vya kipindupindu vimerekodiwa hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na vifo vya zaidi ya watu 7,000; hilo likiwa ongezeko la zaidi ya 30% ikilinganishwa na mwaka jana.

Ripotii ya Africa CDC imesema, Nchi kama vile Angola na Burundi zimeshuhudia ongezeko kubwa la maambukizi ya kipindupindu katika wiki za hivi karibuni kutokana na upatikanaji mdogo wa maji salama ya kunywa.

Hata hivyo Africa SDC imesema kuna dalili za kuboreka hali ya mambo katika baadhi ya maeneo na kwamba mlipuko wa ugonjwa huo nchini Kongo sasa umedhibitiwa, huku visa vikipungua.

Kupungua maambukizi ya kipindupindu pia kumeonekana Sudan Kusini na Somalia, ingawa maeneo yaliyoathiriwa na migogoro yanabaki kuwa hatarini zaidi huku kambi zilizojaa watu wengi zenye usafi duni zikiongeza kasi ya maambukizi.

Kipindupindu, ni ugonjwa wa kuhara unaoenea haraka na unaoweza kusababisha kifo. Ugonjwa huo hustawi pale ambapo mifumo ya maji taka huwa dhaifu na vyanzo vya maji vimechafuliwa kwa kinyesi.

Wakati huo huo, mamlaka nchini Ethiopia zimegundua visa vinane vinavyoshukiwa kuwa vya homa ya kutokwa na damu (hemorrhagic fever) inayosababishwa na virusi na zinasubiri matokeo ya vipimo, huku timu za mwitikio wa haraka zikifanya kazi ili kudhibiti tishio hilo.

CDC Africa pia imeeleza kwamba ingawa mlipuko wa Mpox unapungua katika baadhi ya mataifa yaliyoathiriwa sana, lakini unaendelea kusababisha hatari katika nchi za Kenya, Guinea, Liberia na Ghana.