Wanajeshi watano wa Misri wauawa katika eneo la Sinai
Wanajeshi watano wa Misri wameuawa katika shambulio lililofanywa na watu wenye silaha katika eneo la Sinai la kaskazini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Duru za kijeshi za Misri zimesema kwamba watu wenye silaha jana Jumamosi waliwashambulia wanajeshi wa nchi hiyo katika mji wa Sheikh Zuweid ulioko katika Peninsula ya Sinai na kuua wanajeshi watano.
Habari zaidi zinasema kuwa, askari sita waliojeruhiwa katika shambulio hilo la jana wamepelekwa katika hospitali ya kijeshi iliyoko katika mji wa bandari wa al-Arish.
Polisi na wanajeshi wa Misri wamekuwa wakishambuliwa mara kwa mara na watu wenye silaha ambao wana maficho yao mengi kaskazini mwa Misri.
Ngome za magenge hayo ziko katika mkoa wa Sinai Kaskazini ambapo kundi hatari zaidi kuliko yote ni lile linalojiita Answar Bayt al Muqaddas ambalo limetangaza rasmi utiifu wake wa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) na limebadilisha jina na kujiita Wilayat Sinai.
Mkoa wa Sinai wa kaskazini mwa Misri umekuwa uwanja wa mapigano baina ya maafisa usalama na magenge ya kigaidi ambayo yameshadidisha mashambulizi yake katika miaka ya hivi karibuni, hususan baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali halali ya nchi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Mohammad Morsi hapo mwaka 2013.