Amnesty yaitaka serikali ya Misri kuwafikisha mahakamani maafisa waliofanya mauaji ya Rabi'a
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa serikali ya Misri ilifumbia macho suala la kuwafikisha mahakamani maafisa na askari usalama waliohusika na mauaji ya raia wasiopungua 900 wakati wa kuvunja mgomo wa wananchi kwa kutumia mabavu katika medani za Rabi'a al-Adawiyya al Nahdha mwaka 2013.
Taarifa hiyo ya Amnesty International imetolewa kwa mnasaba wa kukumbuka mauaji hayo na ukandamizaji wa raia waliokuwa wakifanya mgomo katika Medani ya Rabi'a al-Adawiyya mjini Cairo tarehe 14 Agosti mwaka 2013. Raia hao walikuwa wakipinga hatua ya jeshi la Misri ya kumuondoa madarakani Muhammad Mursi aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasia kuwa rais wa nchi hiyo.
Naibu Mkurugenzi wa Amnesty international kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, Lynn Maalouf amesema kuwa, hukumu ya kifo iliyotolewa kwa raia 12 na vifungo vya mamia ya wengine kwa madai ya kuhusika katika mauaji hayo ni kielelezo cha vipaumbele vinavyotia shaka vya kile kinachotajwa kuwa ni mfumo wa uadilifu nchini Misri.
Amnesty international imeitaka serikali ya Misri kufuta hukumu hiyo na kukomesha mtindo wa kutumia adhabu ya kifo kama silaha dhidi ya wapinzani wa kisiasa ili kueneza hofu na wahka katika jamii.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu pia limeitaka Misri kuwafikisha mahakamani wahusika halisi wa mauaji ya Rabi'a al-Adawiyya na al Nahdha.
Amnesty International pia imeitaka jamii ya kimataifa kuzidisha mashinikizo dhidi ya Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri ili akomeshe adhabu ya kifo dhidi ya wapinzani.
Duru za kuaminika zinasema zaidi ya raia elfu moja waliuawa kwa kupigwa risasi wakati askari usalama wa serikali ya Cairo walipovamia maandamano ya amani katika Medani ya Rabia al Adawiyya na mengine katika eneo la Giza.
Wamisri wanayatambua mauaji ya Medani ya Rabi'a al-Adawiyya kuwa ndiyo makubwa zaidi katika historia ya sasa ya nchi hiyo.
Amnesty International inasema, hadi sasa hakuna afisa yeyote aliyechukuliwa hatua kutokana na mauaji hayo ya Rabi'a al-Adawiyya.