Odinga asema Wakenya watajutia uamuzi wa Mahakama ya Rufaa wa kukataa BBI
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73990-odinga_asema_wakenya_watajutia_uamuzi_wa_mahakama_ya_rufaa_wa_kukataa_bbi
Kiongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga amesema kugonga mwamba mchakato wa kurekebisha Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) kutakuwa na taathiri mbaya kwa mandhari ya kijamii na kisiasa ya Kenya katika siku zijazo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 27, 2021 07:37 UTC
  • Raila Odinga
    Raila Odinga

Kiongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga amesema kugonga mwamba mchakato wa kurekebisha Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) kutakuwa na taathiri mbaya kwa mandhari ya kijamii na kisiasa ya Kenya katika siku zijazo.

Odinga anasisitiza kuwa mabadiliko yaliyosimamishwa ya Katiba yalikuwa na nia nzuri kwa nchi ya Kenya.

Odinga ambaye alikuwa akizunumza na vyombo vya habari mapema leo Ijumaa amesema: "Kwa sababu ya ufinyu wa wakati, sasa tumeamua kusitisha mchakato huo kwa muda ili kuwapa Wakenya muda wa kujadiliana juu yake." 

Amesisitiza kuwa "Kenya itajuta kutokana na uamuzi wa korti wa kutupilia mbali mchakato wa BBI."

Siku chache zilizopita Mahakama ya Rufaa nchini Kenya, iliunga mkono uamuzi wa Mahakama Kuu, kuwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini humo maarufu kama BBI, ni kinyume cha Katiba ya nchi hiyo na kutupilia mbali rufaa iliyowasilishwa kutaka maamuzi hayo yatenguliwe.

Majaji sita kati ya saba wa mahakama hiyo walimshtumu Rais Uhuru Kenyatta kuwa amekwenda kinyume cha Katiba kwa kuanzisha mchakato huo.

Baadaya uamuzi huo Bw Odinga alitoa taarifa akisema chama cha ODM hakitaelekea katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, lakini alidokeza kuwa suala la kutaka marekebisho ya katiba halijafika kikomo.

Raila Odinga

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema, baadhi ya masuala yaliyopendekezwa katika BBI huenda yakapitishwa bungeni huku mengine yakifufuliwa baada ya 2022, hasa ikiwa waziri huyo mkuu wa zamani atafanikiwa kuunda serikali ijayo.

Miongoni mwa mapendekezo ya BBI ambayo huenda yakapitishwa katika Bunge la Kenya ni lile linalotaka mawaziri wawe wakichaguliwa kutoka miongoni mwa wabunge, na vilevile, magavana waruhusiwe kuchagua mawaziri wa kaunti kutoka miongoni mwa madiwani.

Mchakato wa kutaka kuibadilisha Katiba ya nchi hiyo iliyopatikana mwaka 2010, ulianza baada ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, kumaliza uhasama wao kisiasa na kuungana ili kubadilisha mfumo wa uongozi nchini humo.