Rais wa Misri afuta sheria ya hali ya hatari
(last modified Tue, 26 Oct 2021 07:55:20 GMT )
Oct 26, 2021 07:55 UTC
  • Rais wa Misri afuta sheria ya hali ya hatari

Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri ametangaza kuwa serikali yake imetengua sheria ya hali ya hatari kitaifa nchini humo.

Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minne kwa serikali ya Cairo kufuta sheria hiyo, ambayo ilitangazwa kwa mara ya kwanza mnamo Aprili mwaka 2017, baada ya kujiri mashambulio ya kigaidi yaliyolenga makanisa ya Wakristo wa Kikhufti (Coptic).

Katika ujumbe kupitia mtandao wa Twitter, Sisi amesema, Misri hivi sasa ni kisiwa cha amani na uthabiti katika eneo, huku akiwashukuru wananchi wazalendo wa nchi hiyo kwa jitihada zao. 

Rais huyo amekuwa akitumia visingizo mbalimbali kurefusha muda wa hali ya hatari nchini Misri, likiwemo janga la Corona.

Katika miezi ya karibuni, asasi nyingi za kimataifa na za kutetea haki za binadamu zimetoa indhari kuhusu utendaji wa utawala wa Misri unaoongozwa na Sisi katika masuala ya uhuru wa kijamii na kisiasa na ukiukaji wa haki za binadamu.

Maafisa usalama Misri

Baada ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali halali na ya kidemokrasia ya Muhammad Morsi, Sisi alishika hatamu za utawala nchini Misri kufuatia uchaguzi wa kimaonyesho wa rais uliofanyika mwaka 2014.

Tangu wakati huo hadi sasa na kwa kutegemea uungaji mkono wa Magharibi, rais huyo wa Misri amekuwa akitekeleza sera ya ukandamizaji dhidi ya wapinzani na wakosoaji wa utawala wake.

Tags