Jenerali al Burhan alitembelea Misri kwanza kabla ya kufanya mapinduzi Sudan
Gazeti moja la nchini Marekani limefichua kuwa, kamanda wa jeshi la Sudan alitembelea Misri siku moja tu kabla ya kuongoza mapinduzi ya kijeshi nchini Sudan.
Gazeti la Wall Street Journal la nchini Marekani limefichua habari hiyo na kusema kuwa, Jenerali Abdul Fattah al Burhan alionana na mkuu wa shirika la kijasusi la Misri katika ziara yake hiyo ya siri na aliporejea Sudan aliongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyioing'oa madarakani serikali ya mpito iliyokuwa inawashirikisha pia raia.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Marekani, al Burhan alielekea nchini Misri baada ya kufanya mazungumzo na Jeffrey David Feltman, mjumbe maalumu wa Marekani katika eneo la Pembe ya Afrika.
Wall Street Journal limefichua mambo yanayoonesha kuweko baraka kamili za Marekani, Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel kabla ya Jenerali Abdul Fattah al Burhan kufanya mapinduzi ya kijeshi, kumtia mbaroni Waziri Mkuu wa Sudan, Abdullah Hamdok na kumuweka kwenye kifungo cha nyumbani.
Duru tatu za kuaminika zimeliambia gazeti hilo la Marekani kwamba, katika mazungumzo yake na Jenerali al Burhan, Abbas Kamil, mkuu wa shirika la kijasusi la Misri alimweleza kamanda huyo wa jeshi la Sudan kuwa Cairo haifurahishwi na misimamo ya Waziri Mkuu wa Sudan, Abdullah Hamdok. Baada ya hapo Jeneral al Burhan alifanya mapinduzi na kuivunja serikali ya Hamdok na kuwatia mbaroni mawaziri na maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa serikali hiyo akiwemo Waziri Mkuu mwenyewe, Abdullah Hamdok.