Umoja wa Mataifa wazitaka Algeria na Morocco kupunguza mzozo baina yao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i76628-umoja_wa_mataifa_wazitaka_algeria_na_morocco_kupunguza_mzozo_baina_yao
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitolea wito Algeria na Morocco kufanya juhudi za kupunguza mzozo na mivutano baina yao.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Nov 07, 2021 04:03 UTC
  • Umoja wa Mataifa wazitaka Algeria na Morocco kupunguza mzozo baina yao

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezitolea wito Algeria na Morocco kufanya juhudi za kupunguza mzozo na mivutano baina yao.

Hayo yameelezwa na msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa baada ya kushadidi hitilafu baina ya Morocco na Algeria, ambapo Farhan Haq amesema kuwa, Antonio Guterres amezitaka Algiers na Rabat kufanya mazungumzo ili kuzipatia ufumbuzi hitilafu na tofauti zilizoibuka baina ya mataifa hayo mawili ya Kiarabu. 

Hivi karibuni serikali ya Algeria ilitangaza kuwa, imeifungia Morocco anga yake hatua ambayo ilizidi kuchochea mvutano ulioshadidi hivi karibuni baina ya majirani hao wawili kufuatia hatua ya Algiers ya kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Rabat.

 Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa 

 

Mwishoni mwa mwezi uliopita Morocco ilimwita nyumbani balozi wake aliyekuwa akiiwakilisha nchi hiyo katika nchi jirani ya Algeria baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria kuzituhumu taasisi za serikali ya Morocco kuwa zinahusika katika kufadhili na magendo ya bangi.

Tukio la moto mkubwa uliosambaa kwenye misitu ya Algeria ambalo lilisababisha vifo vya watu wasiopungua 90 na kuwajeruhi wengine wengi na sisitizo la viongozi wa Algiers kwamba ajali hiyo ilisababishwa makusudi kwa kuhusisha makundi ya kigaidi, linatajwa kuwa, limeshadidisha hali ya mvutano iliyokuwepo baina ya nchi hiyo na Morocco.

Aidha hatua ya serikali ya Morocco ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel inaelezwa kuwa, sababu nyingine ya kuharibika uhusiano baina ya nchi mbili hizo kwani Algeria imechukizwa mno na kitendo cha jirani yake huyo.