Mwanadiplomasia wa zamani: Israel na Misri ziliunga mapinduzi ya kijeshi Sudan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Zamani wa Sudan amesema kuwa, Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel ziliunga mkono mapinduzi ya kijeshi nchini mwake.
Shirika la habari la FARS limemnukuu Balozi Maryam al Mahdi akisema hayo na kuongeza kuwa, mapinduzi ya hivi karibuni ya kijeshi yaliyotokea nchini Sudan na ambayo yamepingwa na nchi zilizo nyingi duniani, yalikuwa na baraka kamili za utawala wa Kizayuni na Misri.
Amesema, mapatano yaliyofikiwa hivi sasa baina ya Jenerali Abdul Fattah al Burhan, kamanda wa jeshi la Sudan na Abdulla Hamdok, Waziri Mkuu wa Sudan aliyepinduliwa, hayakubaliki.
Jumapili wiki hii, televisheni ya serikali ya Sudan ilitangaza kuwa, Abdul Fattah al Burhan na Abdullah Hamdok wamefikia makubaliano maalumu yenye vipengee 14 na ndiyo yaliyomrejesha madarakani Hamdok kama Waziri Mkuu wa Sudan siku ya Jumatatu.
Tarehe 25 Oktoba mwaka huu, Jenerali Abdul Fattah al Burhan aliongoza mapinduzi ya kijeshi yaliyoing'oa madarakani serikali ya mpito ambayo ilikuwa inashirikisha pia raia huko Sudan. Kabla ya jambo lolote, wanajeshi walioongozwa na al Burhan walimtia mbaroni Waziri Mkuu Abdullah Hamdok, baadaye wakaivunja serikali yake na kuwaweka kizuizini watu wengi.
Hata hivyo maandamano ya kila siku ya wananchi ambayo maafisa wa kijeshi na polisi walikuwa wanawafyatulia watu risasi hai kujaribu kuwatawanya, yamewalazimisha majenerali wa kijeshi wamrudishe madarakani Waziri Mkuu Hamdok.
Pamoja na hayo wapinzani na wananchi wa Sudan wanaendelea na maandamano wakiwataka wanajeshi warejee kwenye kambi zao na waruhusu demokrasia inayoheshimu matakwa ya wananchi ifuate mkondo wake nchini humo.