Hospitali Zimbabwe zakumbwa na upungufu wa wauguzi baada ya mamia kuhamia Uingereza
Ripoti kuhusu upungufu wa wauguzi katika hospitali za serikali na za binafsi huko Zimbabwe zimeendelea kugonga vichwa vya habari katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, mamia ya wauguzi wamehama na kuelekea Uingereza, Ireland na katika nchi jirani kama Afrika Kusini kwa ajili ya kutafuta maisha bora.
Taarifa zinasema kuwa, katika miezi ya karibuni baadhi ya hospitali za serikali na za sekta binafsi zimekuwa zikitoa huduma kwa asilimia 50 ya wagonjwa.
Itakumbwa kuwa, Uingereza imekuwa ikijaribu kuwaajiri wafanyakazi wa sekta ya afya kutoka nchi mbalimbali ili kuongeza idadi ya wataalamu wake wa afya ambao waliathiriwa na janga la COVID-19 na Brexit.
Kwa mujibu wa Bodi ya Huduma za Afya ya Zimbabwe, zaidi ya wafanyakazi wa afya 2,200 wakiwemo wauguzi 900, waliacha kazi nchini humo mwaka uliopita wa 2021. Idadi hiyo ni mara mbili ya wafanyakazi wa sekta ya afya walioacha kazi mwaka juzi wa 2020 na kuelekea nje ya nchi; na ni mara tatu ya walioacha kazi mwaka mmoja kabla yake.

Wauguzi yaani manesi nchini Zimbabwe hulipwa mishahara midogo huku kiwango cha chini kikitajwa kuwa dola 200; ambazo hata hivyo hazitoshi kukidhi mahitaji ya maisha katika nchi iliyoathirika na mfumuko mkubwa wa bei katika muongo mmoja uliopita.