Raila avunja kimya, awapongeza majaji waliokomesha mchakato wa BBI
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i82026-raila_avunja_kimya_awapongeza_majaji_waliokomesha_mchakato_wa_bbi
Kinara wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga amevunja kimya chake kufuatia uamuzi uliotolewa jana Alkhamisi na Mahakama ya Juu ya Kenya kuwa BBI sio halali na haikuzingatia sheria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 01, 2022 05:56 UTC
  • Raila Odinga
    Raila Odinga

Kinara wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga amevunja kimya chake kufuatia uamuzi uliotolewa jana Alkhamisi na Mahakama ya Juu ya Kenya kuwa BBI sio halali na haikuzingatia sheria.

Raila aliyeongoza muswada wa maridhiano wa BBI akiwa pamoja na Rais Uhuru Kenyatta, amesifia uamuzi uliotolewa na majaji saba wa mahakama hiyo siku ya Alhamisi Machi 31. Waziri mkuu huyo wa zamani wa Kenya amesema uamuzi uliotolewa umezingatia uhuru wa Wakenya na kutilia mkazo kwamba idara za Serikali zinapaswa kuwajibikia wananchi wa taifa hili.

Raila anayewania wadhifa wa urais kwa tikiti ya vuguvugu la Azimio la Umoja amempongeza Jaji Mkuu Martha Koome, kuhusu tamko lake la majukumu ya Idara ya Mahakama, ikilinganishwa na yale ya afisi ya Rais na Bunge.

Raila amesema asasi tatu za dola zinapaswa kufuatiliwa kwa karibu, ili kuimarisha muongozo kwa minajili ya kutekeleza malengo ya kikatiba.

Uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Kenya unakomesha kabisa matumaini matumaini ya kufufua mpango wa maridhiano wa BBI. Katika uamuzi uliotolewa, majaji wa mahakama hiyo walikubaliana kwa kauli moja na Mahakama Kuu na ile ya rufaa kupinga mchakato huo.

Mahakama hiyo imesema Rais Uhuru Kenyatta ndiye aliyeanzisha mchakato wa BBI ilhali hana ruhusa kisheria kufanya hivyo.

Kenyatta na Odinga

Mchakato wa BBI ulikuwa na lengo ya kurekebisha Katiba kupitia maridhiano ya kitaifa.

Miongoni mwa mapendekezo ya BBI ambayo huenda yakapitishwa katika Bunge lijalo la Kenya ni lile linalotaka mawaziri wawe wakichaguliwa kutoka miongoni mwa wabunge, na vilevile, magavana waruhusiwe kuchagua mawaziri wa kaunti kutoka miongoni mwa madiwani.

Mchakato wa kutaka kuibadilisha Katiba ya nchi hiyo iliyopatikana mwaka 2010, ulianza baada ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, kumaliza uhasama wao kisiasa na kuungana ili kubadilisha mfumo wa uongozi nchini humo.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema, baadhi ya masuala yaliyopendekezwa katika BBI huenda yakapitishwa bungeni huku baada ya 2022, hasa ikiwa waziri huyo mkuu wa zamani atafanikiwa kuunda serikali ijayo.