Mripuko wa kipindupindu waikumba Cameroon, kesi 6,000 zaripotiwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i82060-mripuko_wa_kipindupindu_waikumba_cameroon_kesi_6_000_zaripotiwa
Watu wasiopungua 100 wamepoteza maisha kutokana na mripuko mpya wa kipindupindu nchini Cameroon, huku wengine 6,000 wakikumbwa na ugonjwa huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2022 08:27 UTC
  • Mripuko wa kipindupindu waikumba Cameroon, kesi 6,000 zaripotiwa

Watu wasiopungua 100 wamepoteza maisha kutokana na mripuko mpya wa kipindupindu nchini Cameroon, huku wengine 6,000 wakikumbwa na ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ya nchi hiyo, maradhi hayo yameshaenea katika asilimia 40 ya miji mikubwa ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Yaoundé. Miji mingine iliyoathiriwa zaidi kwenye mripuko wa sasa wa maradhi hayo ni pamoja na Douala, Buea, Limbe na Bafoussam.

Waziri wa Afya wa Cameroon, Manaouda Malachie ametadharisha kuwa, Gereza la New Bell katika mji mkuu wa kiuchumi wa Doula ndicho kitovu cha mripuko wa hivi sasa wa kipindupindu, huku akisisitiza kuwa wamechukua hatua stahiki kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo katika maeneo mengine ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Naye Gaston Eloundou Essomba, Waziri wa Maji wa nchi hiyo ameiagiza Kampuni ya Kusambaza Maji nchini humo kuhakikisha kuwa maji safi na salama yanamfikia kila mtu katika miji na vijiji vilivyokumbwa na mripuko huo.

Ramani ya Cameroon

Miripuko ya maradhi hayo hatarishi huripotiwa nchini humo na katika nchi nyingine za Afrika Magharibi mara kwa mara, hususan katika misimu ya mvua za masika zinazoambatana na mafuriko.

Takwimu zinaonesha kuwa, kwa wastani kesi milioni 2.8 za maradhi hayo huripotiwa kila mwaka katika pembe mbali mbali za dunia, mbali na vifo zaidi ya 91,000. Ugonjwa wa kipindupindu husababishwa na baktria waitwao Vibrio cholera na huenezwa kwa kunywa maji yasiyo salama. Dalili za ugonjwa huo ni maumivu ya tumbo, kuharisha, kutapika pamoja na homa.