Miili 4,000 ya wahanga wa ukatili wa Wafaransa yagunduliwa nchini Algeria
Waziri wa "Wanajihadi" wa Algeria ametangaza habari ya kugunduliwa visima chungu nzima vyenye miili 4,000 ya watu waliouliwa na wakoloni wa Ufaransa wakati wanajihadi wa Algeria walipoendesha mapambano makali dhidi ya wavamizi hao makatili wa Ulaya.
Shirika la habari la FARS limemnukuu waziri huyo akisema kuwa, katika mikoa 12 ya Algeria kumegunduliwa visima kuanzia kimoja hadi vitatu katika kila mkoa na kila kisima kilikuwa na miili baina ya 10 hadi 400 ya watu waliouliwa kikatili na wakoloni hao wa Ulaya.
Waziri huyo wa Algeria ameongeza kuwa, faili la watu waliotoweka wakati wa "Vita vya Ukombozi" wa nchi hiyo limethibitisha kuwa Waalgeria hao walikuwa wanauliwa kikatili na kutumbukizwa visimani ili kupoteza ushahidi kikamilifu. Amesema, mafaili hayo ni katika orodha ya mauaji mabaya sana ya kikatili yaliyofanywa na wakoloni hao wa Ufaransa dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Algeria.
Wananchi wa Algeria ni maarufu duniani kwa kuendesha mapambano ya kishujaa dhidi ya mkoloni kizee wa Ulaya yaani Ufaransa. Wananchi hao waliendesha mapambano ya ukombozi kwa muda wa miaka 132 hadi walipowatimua wavamizi hao waliofanya ukatili mkubwa mno dhidi ya wananchi wa Algeria.
Katika kipindi cha miaka ya baina ya 1954 hadi 1962, Wafaransa waliua kikatili na kinyama zaidi ya Waalgeria milioni moja.
Jinai hizo za mkoloni huyo kizee wa Ulaya nchini Algeria zilikuwa kubwa kiasi kwamba, Wafaransa hao waliwafanyia mpaka majaribio ya nyuklia wananchi wa maeneo mbalimbali ya Algeria kwa kuwaweka moja kwa moja mbele ya mionzi ya silaha hatari za nyuklia ili kuona taathira zake.