WFP: Njaa inatishia maisha ya watu milioni 22 barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i87260-wfp_njaa_inatishia_maisha_ya_watu_milioni_22_barani_afrika
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limessema kuwa hivi sasa watu milioni 22 barani Afrika wako kwenye hatari ya kupoteza maisha kutokana na baa la njaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 21, 2022 02:28 UTC
  • WFP: Njaa inatishia maisha ya watu milioni 22 barani Afrika

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP limessema kuwa hivi sasa watu milioni 22 barani Afrika wako kwenye hatari ya kupoteza maisha kutokana na baa la njaa.

Ofisi ya barani Afrika ya WFP imetoa ripoti mpya jijini Nairobi Kenya na kuongeza kuwa, shirika hilo limeamua kudhamini misaada ya chakula kwa bara la Afrika kutokana na kuongezeka sana watu waliokumbwa na baa la njaa hasa kutokana na ukame wa miaka mingi mfululizo.

Shirika hilo limesema, watu wapatao milioni 345 katika nchi 82 duniani wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Kwa mujibu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, watu milioni 50 kutoka nchi 45 wako kwenye ukingo wa baa la njaa na wana hatari ya kutumbukia kwenye hali mbaya zaidi iwapo misaada wa kibinadamu haitowafikia haraka. 

Ukame na ukosefu wa mvua wa muda mrefu, moja ya sababu ya janga la njaa barani Afrika

 

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya ofisi ya WFP ya jijini Nairobi Kenya, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022, watu milioni 9 wameongezeka katika orodha ya watu wasio na usalama wa chakula barani Afrika. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi zilizoathirika zaidi na Ethiopia, Kenya na Somalia. Kuongezeka idadi hiyo kubwa ya watu wasio na usalama wa chakula barani Afrika kumeifanya idadi ya watu wanaohitajia mno misaada hiyo barani Afrika na kufikia milioni 22.

Hii ni katika hali ambayo, meli yenye jina la MV Brave Commander iliondoka bandari ya Bahari Nyeusi ya Pivdennyi nchini Ukraine wiki iliyopita kuelekea nchini Djibouti ikiwa na shehena kubwa ya nafaka kwa ajili ya Ethiopia. Meli hiyo imebaba tani 23,000 ka ajili ya watu wenye mahitaji makubwa ya chakula nchini Ethiopia chini ya mpango maalumu wa Umoja wa Mataifa.