Hofu ya UN juu ya mgogoro wa kisiasa nchini Libya
Mkuu wa Siasa wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa, kutotatuliwa mgogoro wa kisiasa wa Libya na kutofanyika uchaguzi uliocheleweshwa ni tishio kwa hali ya mambo katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Rosemary DiCarlo ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, mgogoro wa sasa umetokana na kushadidi mvutano wa kisiasa kati ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa GNU inayoongozwa na Waziri Mkuu wake Abdul Hamid Al-Dabibah na serikali iliyopewa mamlaka na bunge lenye makao yake mjini Tabruk mashariki ya nchi ambayo inaongozwa na Fathi Bashagha.
DiCarlo ameeleza bayana kuwa, mzozo huo ulioanza Agosti 27 linaonekana kuwa jaribio la vikosi vitiifu kwa Bashagha kuingia katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Afisa huyo wa UN amezitaka pande hasimu kwenye mzozo huo kuzingatia maslahi ya taifa, usalama wa wananchi na kutatua mambo yao kwa njia ya mazungumzo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imeziasa pande zote hasimu kuvumiliana na kujizuia kuwasha moto zaidi wa mapingano na badala yake wazingatie zaidi maslahi ya kitaifa ya wananchi wa Libya.
Kwa mujibu wa mamlaka za Libya, watu wasiopungua 42 wameuawa na wengine zaidi ya 150 wamejeruhiwa katika mapigano makali yaliyozuka upya mapema Jumamosi iliyopita katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.