Nchi 80 zalaani mpango wa Israel wa kughusubu Ukingo wa Magharibi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i136760-nchi_80_zalaani_mpango_wa_israel_wa_kughusubu_ukingo_wa_magharibi
Zaidi ya nchi 80 wanachama wa Umoja wa Mataifa zimelaani mpango wa Israel wa kupora na kuyakalia kwa mabavu maeneo kadhaa ya ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu, na kuyatambua maeneo hayo ya Palestina kama "milki ya serikali" ya Israel.
(last modified 2026-02-18T06:25:44+00:00 )
Feb 18, 2026 06:25 UTC
  • Nchi 80 zalaani mpango wa Israel wa kughusubu Ukingo wa Magharibi

Zaidi ya nchi 80 wanachama wa Umoja wa Mataifa zimelaani mpango wa Israel wa kupora na kuyakalia kwa mabavu maeneo kadhaa ya ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu, na kuyatambua maeneo hayo ya Palestina kama "milki ya serikali" ya Israel.

"Tunalaani vikali maamuzi na hatua za upande mmoja za Israel zinazolenga kupanua uwepo haramu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi," Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour alisema hayo jana Jumanne, akizungumza kwa niaba ya muungano wa nchi 85 na mashirika kadhaa ya kimataifa.

"Maamuzi kama hayo ni kinyume na wajibu wa Israel chini ya sheria za kimataifa na lazima yabatilishwe mara moja. Tunabainisha upinzani wetu mkubwa kwa aina yoyote ya unyakuzi," Mansour amesema.

Nchi zilizosaini taarifa hiyo ya pamoja jana Jumanne ni pamoja na Australia, Canada, China, Ufaransa, Pakistan, Russia, Korea Kusini, Saudi Arabia, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu, Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC.

Kabla ya hapo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, HAMAS ilitoa taarifa ikilaani mpango huo, na kuuelezea uamuzi huo kuwa ni jaribio la kutwisha maamuzi ya kivamizi na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Aidha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali uamuzi wa hivi karibuni wa utawala ghasibu wa Israel wa kunyakua ardhi zaidi za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ikisema hatua hiyo inalenga kupanua 'ujenzi wa vitongoji haramu' na kuimarisha uvamizi na udhibiti wa masuala ya usalama katika eneo hili, sambamba na kuendeleza 'mauaji ya kimbari' Gaza.

Radiamali hizo za nchi 80 wanachama wa UN, Hamas, wadau wa kikanda na serikali mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Iran, Bunge la Kiarabu, na Wizara za Mambo ya Nje za Qatar na Misri, zinasisitiza kuwa, mpango huo wa utawala wa Kizayuni utakuwa na matokeo makubwa hasi si tu kwa Palestina, bali kwa eneo lote la Asia Magharibi.