Algeria yataka utawala wa Kizayuni uondoke kwenye milima ya Golan ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i88644-algeria_yataka_utawala_wa_kizayuni_uondoke_kwenye_milima_ya_golan_ya_syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria kwa mara nyingine tena ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ukomeshe kuikalia kwa mabavu milima ya Golan ya Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 27, 2022 23:22 UTC
  • Algeria yataka utawala wa Kizayuni uondoke kwenye milima ya Golan ya Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria kwa mara nyingine tena ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ukomeshe kuikalia kwa mabavu milima ya Golan ya Syria.

Mara kwa mara wanajeshi wa Utawala wa Kizayuni wanaingia bila ya ruhusa katika anga ya Lebanon kutokea milima ya Golan na kwenda kufanya mashambulio katika maeneo ya mashariki na kaskazini magharibi mwa Syria.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu  Ramtane Lamamra, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria akisema hayo na kuongeza kuwa, utawala wa Kizayuni lazima uondoke kwenye milima ya Golan ya Syria unayoikalia kwa mabavu kama yanavyohimiza maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Ramtane Lamamra, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria

 

Amma kuhusu utawala wa Kizayuni kuendelea kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina, Lamamra amesema, utatuzi wa kadhia ya Palestina ndiyo njia pekee ya kuweza kupatikana amani na utulivu katika eneo la Asia Magharibi. Jambo hilo haliwezekani mpaka taifa la Palestina lipewe haki zake na kuundwe nchi huru ya Palestina katika mipaka ya mwaka 1967.

Milima ya Golan ni sehemu ya mkoa wa al Qunaitra wa kusini magharibi mwa Syria. Sehemu kubwa ya eneo hilo ilitekwa na utawala wa Kizayuni katika vita vya siku sita vya 1967 na tarehe 14 Disemba 1981, iliingizwa kinyume cha sheria katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel. Hata hivyo jamii ya kimataifa yakiwemo maazimio ya Umoja wa Mataifa yanasisitiza muda wote kuwa milima ya Golan ni sehemu isiyotenganishika ya ardhi ya Syria.